Adverts

Jan 17, 2011

PINDA AWAPELEKA NGURUDOTO WAKUU WA MIKOA NA WAKURUGENZI

Awataka watekeleze Hotuba ya Rais Kikwete kwa vitendo
*Awagawa katika cluster za mikoa mitatu mitatu

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka Wakuu wa Mikoa yote nchini kubaini maelekezo yaliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati akizindua Bunge Novemba 18, mwaka jana na kuyapangia mkakati wa utekelezaji ili kuboresha maisha ya Watanzania kwa haraka zaidi.

Ametoa agizo hilo jana usiku (Jumapili, 16 Januari 2011) wakati alipokuwa akifunga mkutano wa kazi wa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Miji na Halmashauri uliofanyika kwenye ukumbi wa St. Gaspar mjini Dodoma.

Waziri Mkuu aliitisha kikao hicho cha kazi kwa sababu viongozi hao walikuwa mjini Dodoma kuhudhuria mkutano mkuu wa ALAT ambao wengi wao ni wajumbe. Wengine waliohudhuria kikao hicho ni baadhi ya wabunge, wenyeviti wa Halmashauri zote nchini, madiwani na watendaji kutoka TAMISEMI.

“Yaliyojadiliwa katika kikao hiki ni shule tosha… hatuna maazimio, ni jukumu la kila mmoja kujifunza kutoka kwa mwenzake iwe ni katika kilimo, elimu, ulinzi na usalama au utunzaji mazingira,” alisema.

“Kitu cha msingi hapa ni hotuba ya Mheshimiwa Rais, chukua maelekezo, yapangie mkakati wa utekelezaji, tafuta mbinu za kufikia huo mkakati na uweke ratiba ya kutekeleza kila elekezo…” alisema na kuongeza kuwa katika ngazi ya utekelezaji inabidi waangalie ni wizara gani inasimamia eneo lipi.

Aliwataka wajikite pia katika maeneo 10 ambayo ni elimu, kilimo, uwekezaji, mazingira na mgongano wa kimaslahi baina ya Halmashauri na Madiwani. Mengine ni ulinzi na usalama wa raia, maslahi ya madiwani, maeneo maalum ya wafugaji, watumishi kukaa maeneo kwa muda mrefu na kuweka ulinzi maeneo maalum ya mipakani.

Kuhusu elimu, mbali na udahili wa wanafunzi, Waziri Mkuu aliwataka wazingatie ujenzi wa madarasa, upatikanaji wa madawati na ujenzi wa nyumba za walimu wapya. Na ili kupunguza mdondoko wa wasichana  mashuleni, aliwataka wasimamie ujenzi wa mabweni.

Kuhusu kilimo, aliwataka wapime maeneo ya kilimo katika mikoa yao kwani wengi wao hawana takwimu sahihi juu ya ukubwa wa maeneo ya wakulima na matokeo yake ni upotevu wa mbolea ya ruzuku kutokana na matumizi yasiyo sahihi. Alisisitiza juu ya uaminifu wa watumishi wa umma katika masuala ya ruzuku na ubora wa pembejeo zinazoagizwa.

Ili kuhimiza uwekezaji mikoani, Waziri Mkuu aliwashauri wakuu wa mikoa waitishe mikutano ya uwekezaji na kuwagawa katika clusters nane za mikoa mitatu ukiondoa Dar es Salaam ambayo alisema yenyewe ina fursa nyingi zaidi katika eneo hilo.

Alisema clusters hizo zinawaweka pamoja kijiografia, zinazingatia hali ya hewa na aina ya mazao au rasilmali zilizoko kwenye mikoa husika. Aliitaja cluster ya kwanza ambayo inahusisha mikoa ya Morogoro, Pwani na Tanga. Ya pili ni Kilimanjaro, Arusha na Manyara na ya tatu ni Dodoma, Singida na Tabora.

Cluster ya nne alisema ni Lindi, Mtwara na Ruvuma; ya tano ni Iringa, Mbeya na Njombe; ya sita ni Rukwa, Kigoma na Katavi, wakati ya saba ni Geita, Shinyanga na Simiyu na ya nane ni Kagera, Mwanza na Mara.

Akizungumzia kuhusu mazingira, alisema wanayo fursa ya kushirikisha vijana wa kijiweni kwa kuwapa kazi za kumwagilia maua na miti ili kupendezesha miji yao  bali pia aliwataka watendaji wa serikali za mitaa waangalie uwezekano wa kupitisha sheria ya kukataza matumizi ya mifuko ya plastiki kwani inachafua mno mazingira na inachangia kuziba kwa mitaro ya maji machafu.

“Serikali haina budi kuangalia upya suala hili na ikibidi tuanze kutumia mifuko ya karatasi kama ilivyo kwa nchi za wenzetu,” aliongeza.

Vilevile, alisema Serikali itaangalia upya mfumo wa sasa katika Halmashauri ili kupunguza mgongano wa kimaslahi baina ya halmashauri na madiwani. Kuhusu maslahi ya madiwani, alisema Serikali itatazama namna ya kuboresha maslahi yao kwa sababu wao ndiyo wasimamizi wa karibu wa shughuli za maendeleo.

Kwa wafugaji, Waziri Mkuu alisema kuna haja ya kuandaa mpango maalum kwa wafugaji kama ilivyo kwenye kilimo na hasa kutenga maeneo ya mifugo, kuwapa mbegu za majani ya malisho, kujenga malambo na machinjio.

Kuhusu tatizo la watumishi kukaa maeneo fulani kwa muda mrefu, Waziri Mkuu alisema kuna haja ya kuweka maalum ambayo mtumishi atakaa eneo la kazi ili kuepuka watu kujisahau na kuacha kutimiza wajibu wao.

Alisema kuna haja ya kuweka ulinzi maeneo maalum ya mipakani kama Kigoma, Kagera na maeneo ya Bukombe ambako utekaji nyara wa raia yamekuwa ni matukio ya kila siku. “Mikoa ya mipakani  ipewe jicho maalum,” alisema.

Kikao hicho ambacho kiliisha saa 3 usiku, kilihudhuriwa pia na Waziri wa TAMISEMI, Bw. George Mkuchika, Waziri wa Nchi OWM- Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Jumanne Maghembe.

Ends

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU