Umetolewa mwito kwa wastaafu wa utumishi wa umma kwenye ngazi za uongozi, kuendelea kuutumikia umma katika ngazi ya ushauri, kufuatia uzoefu wao wa muda mrefu kwenye utumishi wa umma, hivyo kubakia na uwezo wa kuona zaidi kuliko watumishi wanao waachia uongozi.
Mwito huo, umetolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Philemon Luhanjo, wakati wa hafla ya kumuaga Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bibi Thecla Shangali, pamoja na wastaafu wengine wa tume hiyo, iliyofanyia jana usiku kwenye ukumbi wa Paradise City Club, hapa jijini Dar es Salaam.
Bwana Luhanjo amesema, wastaafu wa utumishi wa umma ni hazina kubwa sana kwa taifa na ujuzi wao na uzoefu wao bado unahitajika sana katika ngazi ya ushauri, hivyo amewashauri viongozi wa utumishi wa umma walio madarakani, kuhakikisha wanaitumia hazina hii, kwa kuwatumia wastafu wao kwa huduma za ushauri, ‘consultancy’ kila watakapo ona hali inaruhusu.
Kwa upande wao, Katibu Mstaafu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bibi Thecla Shangali, akizungumza kwa niaba ya wastaafu wenzake, alisisitiza kuwa tayari wakati wowote, kuendelea kuipa Tume ya Utumishi, ushauri wake kila atakapohitajika.
Bibi Shangali, ambae ametumikia utumishi wa umma wa takriban miaka 40, ameasema utumishi wa umma, unakabiliwa na changamoto mbalimbali na kuelezea moja ya changamoto kubwa za watumishi wa umma, ni maslahi duni, ukilinganisha na sekta binafsi.
Amewasisitiza watumishi wa umma, kuongeza bidii katika utendaji wao wa kazi, ili kuleta tija zaidi katika maeneo yao, itakayoongeza mapato ya serikali na kuijengea serikali uwezo wa kuboresha zaidi maslahi yao.
Pamoja na changamoto hiza za maslahi duni serikalini, Bibi Shangali, ameisifu serikali kuwa ndiye mwajiri bora zaidi kwa ajira yenye uhakika (job security),na mwenye mazingira bora kabisa ya kufanyia kazi, (working envirionment), vitu vinavyosababisha watumishi wa umma kufanya kazi kwa moyo wa kujitolea (job satisfaction) na hivyo wengi hata walio kwenye sekta binasfi, kutamani kupata kazi serikalini.
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Jovin Kitambi, alimpongeza Bibi Shangali kwa utumishi uliotukuka wakati Kaimu Katibu wa Tume hiyo, Bw. Donald Ndagula akiahidi kuyaenzi mazuri yote yaliyofanywa na Bi. Shangali, ambaye ndiye muasisi wa Tume hiyo iliyoundwa upya kwa sheria mpya ya Utumishi wa Umma, number 8 ya mwaka 2002.
"