- Isije ikawa ni yale yale ya kukurupuka tu kutoa amri bila hata kufanya upembuzi kwanza na kujua kama amri hizo zinatekelezeka ama la. Katika mlolongo huu, kuna sheria za kupiga watu kukata kuni bila kuwapatia nishati mbadala ya kupikia vyakula vyao (soma HAPA). Kuna amri za kupiga marufuku watu kutotupa takataka hovyo bila kuwawekea sehemu za kutupia taka. Kuna kulazimishana kuongea Kiingereza hata bila kuhakikisha kwamba walazimishwa wana uwezo wa kuongea lugha hiyo. Hakuna kukojoa hovyo sawa lakini je, kuna vyoo ambako watu wanaweza kuchepuka na kwenda kujisaidia wakibanwa? Nalisema hili kwa sababu mwezi wa sita mwaka jana nilizunguka na maganda ya chungwa mfukoni Arusha kwa muda mrefu bila kuona mahali pa kuyatupia. Bila kuwa na vyoo vingi safi, watu hawataacha kukojoa uchochoroni. Na hizi pesa za faini zitakazopatikana, zitatumika kufanyia nini? Naomba zitumike kujengea vyoo vingi vya umma, vyoo ambavyo vitatunzwa vizuri na kuhakikisha kwamba vinafanya kazi!
**********************************************
Atakayetema mate, kujisaidia hovyo kutozwa 50,000/-
Na Hellen Ngoromera
SERIKALI imetangaza mkakati wa kumtoza faini ya sh 50,000 mtu yeyote atakayebainika kutema mate hovyo au kujisaidia barabarani.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dk. Terezya Huvisa, ametangaza hatua hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa operesheni ya usafi itakayoanza kutekelezwa katika jiji la Dar es Salaam na miji mingine kuanzia leo.
“Katika operesheni hii ya kusafisha jiji na miji mingine, mfanyabiashara yeyote atakayebainika kufanya biashara katika eneo chafu atafungiwa biashara yake na kushtakiwa,” alisema Dk. Huvisa.
Alisema hali hiyo imekuwepo kwa muda mrefu hapa nchini hali ambayo husababisha uchafuzi wa mazingira hivyo anaamini kwamba mkakati huo utasaidia kuvipunguza vitendo hivyo.
Alisema Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal, ndiye atakayezindua operesheni hiyo kuanzia asubuhi katika viwanja vya Mnazi Mmoja.
Alisema usafishaji huo wa Jiji utafanywa kwa kuwashirikisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, manispaa zote na wadau wengine.
Aliwataka viongozi wa mitaa (mabalozi) wadau wengine kusimamia usafi kwa umakini katika maeneo yao.
Dk. Huvisa alitaka pia wenye mabasi ya abiria hasa yaendayo mikoani kuweka vyombo vya kutupia taka ndani ya mabasi yao ili kuepuka uchafuzi wa mazingira na atakayekiuka atatozwa faini.
Aliwataka askari wa jiji na polisi kufuatilia suala hilo kwa karibu ili kuwabaini watu watakaokiuka taratibu hizo. Alisema yeye kama kiongozi hana mchezo na mtu yeyote kwani anaamini ataweza kusimamia kwa uimara suala hilo.
Chanzo: Tanzania Daima
"