Adverts

Feb 23, 2011

Muswada wa Katiba Mpya Kutua Bungeni April 2011

Dodoma,8 February 2011 SERIKALI katika kudhihirisha azma yake ya kuitikia mwito wa wananchi wa kuundwa kwa Katiba mpya, imetangaza kuwa itawasilisha bungeni, Muswada wa kuundwa kwa Tume itakayoratibu mchakato wa Katiba hiyo katika mkutano wa Tatu wa Bunge la 10, Aprili mwaka huu. Akisoma Tamko la Serikali bungeni, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema hatua hiyo inatokana na kauli ya Rais Jakaya Kikwete katika salamu za mwaka mpya kwa wananchi, Desemba 31, mwaka jana akiahidi kuitazama upya Katiba ili iendane na miaka 50 ya Uhuru. Waziri Mkuu aliliambia Bunge kwamba, pamoja na kauli hiyo, Rais Kikwete alitoa kauli nyingine ya kusisitiza nia ya Serikali kuanza mchakato wa kuitazama upya Katiba ili kuunda mpya, Februari 5 alipohutubia kilele cha maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa CCM, mjini Dodoma. Rais aliahidi kuunda Tume itakayohusisha pande zote za Muungano, lakini pia wanasiasa, wanasheria, wafanyabiashara, wanataaluma na wananchi kutoka makundi mbalimbali ya kijamii ili kuratibu mchakato huo wa kuitazama upya Katiba. “Muswada utakaowasilishwa bungeni ili kujadiliwa, utahusu majukumu ya Tume, utaratibu utakaotumika kuendesha mchakato wa kupata maoni ya wananchi, namna ya kupata wajumbe wa Tume, kazi ya Tume na masuala mengine ya msingi,” alisema. Alisema, hata bila shinikizo kutoka vyama vya CUF na CHADEMA, Serikali ilikuwa na azma ya kuitazama upya Katiba ili kuifanyia mabadiliko iweze kuendana na umri wa miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania, kwa lengo la kustawisha maisha ya wananchi. Alisema ni kutokana na nia hiyo, ndiyo maana Serikali imekuwa ikiunda tume mbalimbali kuitazama upya Katiba kama ile ya Jaji Francis Nyalali ya mwaka 1991 na ya Jaji Kisanga ya mwaka 1998 kupitia White Paper. “Nia ya Serikali ni kuona inatazama upya Katiba ili kuwa na Katiba itakayowapeleka Watanzania miaka 50 ya Uhuru kwa mafanikio zaidi, kuliko kuendelea kuwa na Katiba ya sasa ambayo ilipatikana tangu wakati nchi yetu inapata Uhuru kutoka kwa Mwingereza,” alisema. Tamko la Serikali limekuja siku moja tu baada ya Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila, juzi kuweka wazi kuwa Bunge halitajadili hoja binafsi zilizotarajiwa kuwasilishwa na baadhi ya wabunge kuhusu kuundwa kwa Katiba mpya ya Tanzania. Katibu wa Bunge alisema hatua hiyo inatokana na kwanza, suala hilo kukiuka Katiba ya sasa na pili utayari wa Serikali kuanza mchakato wa kuitazama Katiba ili kuja na Katiba mpya, kwa kuzingatia kauli za Rais Kikwete. Source:The United Republic Of Tanzania -Prime Minister's Office |News |Muswada wa Katiba mpya kutua Bungeni Aprili