Adverts

Feb 24, 2011

NCHI ZALIA NA MALIPO DUNI KWA ASKARI WA KULINDA AMANI

Balozi wetu wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mh. Ombeni Sefue akiwa katika Mkutano wa Kamati Maalum ya Misheni za Ulinzi wa Amani zinazosimamiwa na Umoja wa Mataifa, katika mkutano huo ajenda iliyotawala ilikuwa ni malipo duni wanayolipwa askari wanaohudumu katika Misheni hizo. Tanzania kupitia mwakilishi wake huyo kama ilivyokuwa kwa nchi nyingine, ilisisitiza kwamba wakati umefika kwa viwango hiyo ambavyo havijarekebishwa kwa takribani miaka 19 kufanyiwa kazi. aliyekaa nyuma yake ni Meja Wilbert Ibuge Mwambata Jeshi katika Ubalozi wa Tanzania Umoja wa Mataifa.
NA MWANDISHI MAALUM, NEW YORK Nchi watoa vikosi vya kijeshi kutekeleza misheni za ulinzi wa amani zinazosimamiwa na Umoja wa Mataifa, zimeutaka Umoja wa Mataifa kuangalia upya viwango vinavyolipwa na UM kwa nchi hizo kufidia gharama za upelekaji vikosi vya nchi hizo katika misheni za UM. Kilio hicho kilitolewa kwa nyakati tofauti na wawakilishi wa nchi 47 wanachama wa Kamati Maalum ya Ulinzi wa Amani ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa maarufu kama C34 mwanzoni mwa mkutano wao unaofanyika New York ulioanza siku ya jumanne na kuendelea hadi Machi 18. Kila mmoja wao na kwa hisia tofauti wamezungumzia kutoridhishwa au kukatishwa tamaa na namna UM unavyolishughulikia suala hilo muhimu. Wajumbe wa Kamati hiyo Maalum wanatoka katika nchi wanachama wa UM wasiopungua 147 ambao nchi zao zinachangia misheni hizo kwa kutoa askari, polisi, vifaa au fedha. Pamoja na mambo mengine,C34 inajadili mafanikio, changamoto na mwelekeo wa baadaye wa shughuli nzima ya ulinzi wa amani Chini ya UM. Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Ombeni Sefue, anasema kuna tatizo kubwa pale linapokuja suala la kuangalia upya viwango wanavyolipwa askari. “Hapa pana tatizo, ni lazima tulikubali na tulishughulikie haraka iwezekanavyo. Haitoshi na wala haipendezi kuwa mwagia sifa kemkem askari wetu kwa kazi nzuri, ilhali wakati huo huo hatuko tayari kuwapatia kile wanachokihitaji na kitakacho wahakikishia usalama wao, ustawi na utekelezaji madhubuti wa jukumu walilopewa kulitekeleza ” anasema Balozi Sefue. Anafafanua zaidi kwa kueleza kuwa, mwaka 1996 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipoupitisha mfumo wa sasa wa marejesho ya zana na vifaa ambavyo nchi wanachama wanavitoa kwa ajili ya operesheni za ulinzi, lengo hilo na kwa mtazamo wa Tanzania lilikuwa siyo kuwagawa nchi wanachama katika makundi ya nchi zinazochangia askari na zinazowalipa askari hao bali lengo lilikuwa ni kuwafanya wawe kitu kimoja. Na kwa sababu hiyo anasema Tanzania imesononeshwa sana na namna Mkutano wa Kamati ya Wataalam ya Kujadili Marejesho ya Vifaa vinavyopelekwa na nchi wanachama kwa ajili ya ulinzi wa amani, Ulivyokamilisha majadiliano yake bila kufikia makubaliano thabiti na muafaka na kupelekea kutofanyika marekebisho muhimu katika marejesho ya gharama ya vifaa hivyo ambayo hufanywa na UM kwa nchi hizo. “Rasimu ya taarifa ya Kamati hiyo iliyotolewa Februari nne mwaka huu, imeonesha kuwa mambo mengi muhimu na ya msingi yameachwa yakielea bila kufikiwa makubaliano. Na hivyo kutozipatia Sekretarieti ya UM na Kamati ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya bajeti mwekeleo na mwongozo wa nini wanatakiwa kufanya” anasisitiza Balozi Balozi Sefue alifafanua zaidi kwa kusema “…hata jambo la muhimu sana kuhusu upitiaji na urekebishaji wa viwango vya malipo kwa askari halikufanyika au halikupewa uzito unaostahili, hivyo kushindwa kabisa kulitolea ufumbuzi. Tunaamini suala hili ni la muhimu na linatakiwa kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi…” Kwa kipindi cha takribani miaka 19 sasa, viwango vinavyotolewa na UM kwa nchi wachangiaji majeshi na polisi kwa ajili ya marejesho ya gharama za upelekaji majeshi na polisi hao ambavyo pia nchi huwalipa askari wake, havijafanyiwa marekebisho Hali hiyo imeleta mvutano mkubwa kati ya nchi zinazotoa raslimali watu (kwa maana ya askari na polisi), nyingi zikiwa ni zile zinazoendelea na nchi zilizoendelea ambazo zenyewe zinachangia kwa ama kutoa fedha, wataalam au zana za kivita. Tanzania inahudumu katika misheni za ulinzi wa amani huko Dafur nchini Sudani ambako inacho kikosi kimoja cha infantria , na Kombania moja ya uhandisi wakati huko Lebanon ziko Kombania mbili za Polisi Jeshi (MP). Aidha Tanzania inachangia kwa kutoa askari polisi, askari magereza na waangalizi wa amani wa kijeshi na maafisa wanadhimu. Aidha, inatoa pia maafisa wa Magereza. Pamoja na kuzungumzia suala la malipo ya askari, Balozi Sefue aliezea pia kuibuka kwa mgawanyo wa kazi usio rasmi katika eneo hilo la ulinzi wa amani chini ya UM, mgawanyo anaosema umejielekeza kwa wale wanaochangia askari kwa upande mmoja na wale wanaochangia wataalamu, fedha na vifaa kwa upande mwingine. Balozie Sefue ametahadharisha kuwa mgawanyo huo hauashirii dalili njema katika suala zima la ulinzi wa amani, ambapo anasema shughuli hiyo inahitaji ushirikiano wa pamoja na wa karibu wa jamii yote ya kimataifa. Katika mkutano huo wajumbe pia walionyesha wasiwasi wao kuhusu kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu dhidi ya askari wa kulinda amani. Wameutaka Umoja wa Mataifa kupitia upya sheria, taratibu na dhana nzima ya jukumu hilo ili kutoa fursa ya kuwaadhibu wale wote watakao hatarisha maisha ya walinzi wa amani wanapokuwa katika utekeleza wa majukumu yao.
"