Adverts

Feb 23, 2011

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari - MAZUNGUMZO IVORY COAST

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wenzake wa Afrika wanaotafuta ufumbuzi wa mzozo wa kisiasa katika nchi ya Afrika Magharibi ya Ivory Coast jana, Jumatatu, Februari 21, 2010, walikutana kwa zaidi ya saa tatu na mmoja wa viongozi wawili waliojitangaza marais wa nchi hiyo.
Rais Kikwete na viongozi wenzake wa nchi kutoka nchi za Mauritania, Chad na Afrika Kusini walikutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Laurent Gbagbo, mmoja wa wanasiasa ambao wamejitangaza kuwa Rais wa Ivory Coast kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Novemba 18, mwaka jana.
Kwa muda mwingi wa mkutano huo katika Ikulu ya Ivory Coast mjini Abidjan, viongozi hao walimsikiliza Mheshimiwa Gbagbo na kumwuliza maswali katika hatua hiyo ya kwanza ya kazi ya ujumbe wa viongozi hao ambao ni kuwasililiza na kuwauliza maswali wadau wote katika mzozo huo ambao umeiacha Ivory Coast ikiwa na marais wawili, Serikali mbili na uwezekano mkubwa kuwapo makundi mawili ya watu wenye silaha na waliko tayari kuzitumia kuwania madaraka ya kuongoza nchi hiyo.
Katika mkutano huo, Mheshimiwa Gbagbo aliwahakikishia viongozi hao kuwa yeye ndiye Rais halali wa Ivory Coast kwa sababu alishinda raundi ya pili ya upigaji kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana nchini humo.
Viongozi hao wako Ivory Coast kutekeleza azimio la Umoja wa Afrika (AU) ambao katika Mkutano wa Wakuu wa nchi za AU mwezi uliopita mjini Addis Ababa, Ethiopia, uliteua kundi la nchi sita za Afrika chini ya uenyekiti wa nchi ya Mauritania kutafuta suluhisho la amani katika Ivory Coast.
Nchi zinazounda kundi hilo chini ya uenyekiti wa Mauritania ni Tanzania, Afrika Kusini, Chad, Burkina Faso, Equatorial Guinea ambayo ndiyo mwenyekiti wa sasa wa AU pamoja na Nigeria ambayo ndiyo Mwenyekiti wa Jumuia ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS).
Nchi hizo zilifanya kikao cha kwanza Jumapili ya wiki hii mjini Nouakchott, Mauritania kabla ya kusafiri kwa kuja mjini Abidjan kukutana na pande zote zinazovutana katika mzozo huo wa kisiasa wa nchi hiyo ya Ivory Coast.
Kutwa nzima ya leo, viongozi hao wamepanga kukutana na makundi ya watu na taasisi mbali mbali za wadau wa suala hilo la Ivory Coast. Miongoni mwa watakaokutana na marais hao leo ni pamoja na Mheshimiwa Alassane Quattara, ambaye kama alivyo Gbagbo, amejitangaza kuwa Rais wa Ivory Coast kufuatia matokeo ya uchaguzi mkuu huo wa mwaka jana na pia naye ameunda Serikali yake.
Makundi mengine yanayokutana na viongozi hao leo ni Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika Ivory Coast, Bwana Choi; wajumbe wa Baraza la Katiba la Ivory Coast, wajumbe wa Jeshi la Ivory Coast, wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Ivory Coast kwa upande wa Mheshimiwa Gbagbo, Mkurugenzi wa Sekretarieti ya Serikali ya Mheshimiwa Quattara, na wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Ivory Coast kwa upande wa Mheshimiwa Quattara.
Mikutano mingi inafanyika kwenye Hoteli ya Pullman ambako wamefikia viongozi hao wa Afrika, isipokuwa ile mikutano inayomhusu Mheshimiwa Quattara itakayofanyika kwenye Hoteli ya Golf, mjini Abidjan, ambako kiongozi huyo amejichimbia pamoja na Serikali yake.
Katika raundi ya pili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo ilimtangaza Mheshimiwa Quattara kuwa mshindi.
Lakini Baraza la Katiba ya nchi hiyo lilibadilisha matokeo kwa kutangaza Gbagbo kuwa mshindi baada ya kufuta matokeo ya kura katika majimbo saba ya wilaya 13 za eneo la kaskazini mwa nchi hiyo ambako ndiyo ngome ya Mheshimiwa Quattara.
Hatua hiyo ya Baraza la Katiba ilimpunguzia Mheshimiwa Quattara kiasi cha kura 600,000, sawa na asilimia 12 ya kura zote zilizopigwa.
Mwisho.
Imetolewa na:
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini, Abidjan
Ivory Coast.
21 Februari, 2011
"