Maiti za wagonjwa wa Babu zatupwa porini
Na Peter Saramba, Arusha
IMEBAINIKA kuwa Mzee Piniel Kingori aliyepotea baada ya kupata tiba Loliondo na mwili wake kukutwa umezikwa poririni katika Kijiji cha Ngaresero wilayani Ngorongoro alikufa kwa ajali ya gari na mwili wake kutupwa porini na wafanyakazi wa gari alilokuwa akisafiria.
Mmoja wa ndugu waliokwenda Loliondo kumtafuta mzee huyo na kufanikiwa kupata mwili wake uliozikwa na uongozi wa Wilaya ya Ngorongoro baada ya kutotambulika maeneo yote ya karibu, alisema ilibainika kuwa marehemu alikuwa amevunjika mkono na majeraha kichwani katika ajali iliyohusisha gari aina ya Landcruiser ambalo halikutambulika.
Ndugu huyo Bw. Richard Njavai alisema kwa mujibu wa maelezo waliyopata kutoka kwa wenyeji wa eneo hilo ambalo ni katikati ya pori, pamoja na marehemu kuna watu wengine wawili waliokufa katika ajali hiyo na miili yao kutelekezwa porini na wenye gari pamoja na abiria wengine baada ya kutotambulika.
Katika ajali hiyo walikufa watu watatu ambao ni Mzee King’ori, mama mmoja mwenyeji wa Kilimanjaro ambaye ndugu zake walichukua mwili wake na mtu mwingine aliyedaiwa kuwa ni Mzanzibari ambaye mabaki yake yalichukuliwa na ndugu kwenda kuyazika baada ya kuliwa na wanyama, alisema Bw. Njavai.
Alisema ajali hiyo ilitokea Saa 3 usiku Machi 4, mwaka huu, siku ambayo marehemu King’ori na mwenzake walifika Loliondo na kukutana na foleni kubwa ya kwenda kunywa dawa, hali iliyomlazimu mzee kujipenyeza na kufanikiwa kunywa dawa na kuwaacha wenzake aliokwenda nao, kisha akapanda gari lingine lisilojulikana kurudi Arusha.
Alisema kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Bw. Elias WawaLali, baada ya taarifa za kuwepo miili ya watu waliokufa kupatikana, mwili wa marehemu ulipigwa picha na kusambazwa vijiji jirani ili wananchi wamtambue lakini njia hiyo haikufua dafu ndipo ulipoamuliwa uzikwe Jumatano iliyopita, siku tano baada ya ajali.
Jambo la kusikitisha ambalo ni la kinyama kufanywa na binadamu kwa mwenzake ni kwamba abiria anakufa kwenye ajali na mwili wake unatupwa porini, alisema Bw. Njavai akifuta machozi.
Alishauri serikali iandae utaratibu utakaowezesha abiria wote wanaosafiri kwenda na kutoka Loliondo majina yao kuandikwa ili kudhibiti unyama wa aina hiyo kuendelea kufanyika kwa watu wengine.
Mzee Kingori alizikwa rasmi jana kwa heshima zote katika makaburi ya familia eneo la Kijiji cha Sekei wilayani Arumeru baada ya mwili wake kuletwa usiku wa kuamkia juzi baada ya kufukuliwa na ndugu zake chini ya usimamizi na uratibu wa uongozi wa wilaya ya Ngorongoro na Jeshi la Polisi.
Juhudi za kumtafuta Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Wawa Lali kuzungumzia tukio hilo kwa undani hazikufanikiwa baada ya simu yake ya mkononi kutopatikana.
Source: Majira