Taarifa, ufuatiliaji wa nyendo na hatimaye kukamatwa kwa watuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Rungwe John Mwankenja, ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na maofisa wa idara ya usalama wa taifa imefahamika.
Habari ambazo blog hii imezipata kutoka kijiji cha Ivuna ambako sinema ya kumatwa kwa watuhumiwa hao ilichezwa zinaeleza kuwa wananchi walipigwa na bumbuwazi wakati watuhumiwa hao wanakamatwa kijijini mwao pasipo kujua kama ni sehemu ya mtandao wa wanaoshukiwa na matukio ya uhalifu.
Imeelezwa na wasimuliaji kuwa siku hiyo kuna gari aina ya land cruiser lilifika kijijini kwao na wakashuka watu kadhaa miongoni mwao wakiwa wamevaa ovyo ovyo ambapo wengine walienda kwenye foleni ya matibabu kwenye zahanati ya kata ya Ivuna.
wanaeleza kuwa wengine walikuwa wanahangaika kugonga gari kana kwamba limeharibika na wengine wakijihangaisha na vishughuli mbalimbali vya kijamii , hali ambayo kwa wananchi iliwaachia maswali mengi hasa namna walivyoweza kujichanganya nao na kuendelea kushiriki shughuli hizo.
Inaelezwa kuwa wakati zoezi hilo linaendelea la kujichanganya na wengine wakiwa mafundi wa kutengeneza gari huku wengine wakiendelea na matibabu, mawasiliano yalikuwa yakiendelea baina ya mmoja wa watuhumiwa aliyekuwa mikononi mwao na wenzake waliokuwa wamejificha mahala upande wa ng'ambo.
Taarifa zaidi zinatonya kuwa wakati wakiendelea kuwasiliana, mtuhumiwa huyo alikuwa akiwapa matumaini wenzake kuwa waje wamchukue ili aungane nao, na walipokaribia eneo ambalo alikuwepo ndipo sinema tamu lililofaidiwa na wananchi lilipoanza.
Wananchi wanaeleza kuwa walishangaa wagonjwa waliokuwa kwenye foleni za kumwona daktari na wengine ambao tayari walishafika kwa daktari wakinyanyuka ghafla na kutawanyika kiajabu ajabu ambapo dakika chache hata wale waliokuwa wakitengeneza gari walibadilika ghafla na kuwazingira watu wawili waliokuwa wakija kwa mbele.
Wanaeleza kuwa wakati huo kila mmoja alikuwa ameshika bastola mbili mbili mikononi, hali ambayo wananchi walikuwa wakiona kama video vile kwa jinsi maofisa hao walivyokuwa wepesi katika kuchomoa silaha zao viunoni ambazo hata hivyo kabla hazikushitukiwa na wananchi.
Baada ya filamu hiyo ya dakika chache tayari walikuwa wameshawamudu watuhumiwa kuwewaweka chini ya ulinzi na kuwavisha pingu fasta fasta hatimaye kuwatumbukiza kwenye gari lao.
" yaani ule mchezo mzima haukuzidi dakika mbili manake ilikuwa kama vile wanaigiza sinema lakini ndiyo yanatokea manake jamaa waliruka na kuchomoa vitu viuononi mwao na mara wakawazingira wale jamaa wawili, wakiwa hawajui wafanye nini? anaeleza mmoja wa wananchi.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa idara hiyo ilianza kulifanyia kazi suala hilo tangu lilipotokea kwa kufuatilia taarifa kwa ukaribu na hatimaye kufanikisha kupatikana kwa watuhumiwa hao ambapo mmoja ambaye alipatikana baadaye akiwa amejilaza kwenye gheto mojawapo katika kijiji hicho anayetuhumiwa kuwa ndiye alishika bunduki wakati wa mauaji, pia aliweza kuonyesha wapi ilikokuwa imehifadhiwa.
Inadaiwa kuwa wakati wakirejea na watuhumiwa gari lao liligongwa kwa nyuma na Fuso iliyokuwa imekata breki na kwenda kuwaparamia baada ya askari wa usalama barabarani kulisimamisha gari lao .
Wananchi wameelezea hatua ya utendaji wa idara hiyo ni ya kupongezwa kutokana na jitihada zilizofanywa katika kipindi kifupi na kuwezesha kupatikana taarifa zilizowezesha hadi kuelekezwa mahala ambako siraha hiyo ilikuwa imefichwa na mahala walipo watuhumiwa.
AIDHA mbinu zilizotumiwa na maofisa hao bado zinaelezwa kuwa za kiwango cha juu na hasa namna walivyoweza kuwachanganya wananchi wakati wakiingia kijiji na kuweza kuzoea mazingira ndani ya dakika chache na kujifanya wanakijiji huku wakiwa na mavazi ya kawaida hali ambayo kila mtu hakuweza kubaini kuna wageni zaidi ya kutambua lile gari ambalo lilionekana kama limeleta mgonjwa kwenye zahanati hiyo.
Kazi mmeifanya watu wa intelijensia, nasi kama mabloga tunaungana na wananchi kupongeza kazi hii iliyofanywa kwa staili ya sinema!!!!!! BRAVO BRAVO BRAVO TISS