Adverts

Sep 17, 2011

SHERIA ZA BOXING

PUGILISTIC SYNDICATE OF TANZANIA (PST)
SHERIA ZA BOXING

Na Emmanuel Mlundwa
 
Ulingo wa kupigania:

1       Mapambano yatafanyika ndani ya ulingo wa mraba usiopungua futi 16 x 16na usiozidi futi 20 x 20 kwa ndani.

Kupima uzito, Madaraja ya uzito (Weight classes) na gloves:

2       Mabondia wote ni lazima wapime uzito ili waruhusiwe kupigana. Aidha ubingwa utapangwa kulingana na madaraja ya uzito:

(a)  minimum weight                 47.2 kgs.
(b)  Light Flyweight                  48.89 kgs.
(c)   Flyweight                           50.91 kgs.
(d)  Super flyweight                            52.27 kgs.
(e)   Bantamweight                    53.64 kgs.
(f)    Super bantamweight          55.45 kgs.
(g)  Featherweight                     57.27 kgs.
(h)  Super featherweight           59.09 kgs.
(i)    Lightweight                        61.36 kgs.
(j)    Super lightweight               63.63 kgs.
(k)  Welterweight                      66.67 kgs.
(l)    Super welterweight             70.00 kgs.
(m)Middleweight                      72.72 kgs.
(n) Super middleweight            76.36 kgs.
(o) Light heavyweight              79.54 kgs.
(p) Cruiserweight                     90.00 kgs.
(q) Heavyweight                      +96.6 kgs.

3       Uzito utapimwa siku moja kabla ya siku ya pambano.

4       Inapobidi mabondia watapima uzito siku ya pambano ambapo wanaruhusiwa kuzidi ratili 5 ( 2.3 kgs) juu ya kiwango cha daraja la uzito watakalopigania.

5       Ili liwe pambano la ubingwa ni lazima mmoja wa wapinzani awe na uzito wa daraja lililoidhinishwa. Ubingwa utapewa tu kwa bondia yule aliyefikisha uzito huo iwapo atashinda pambano hilo.  

6       Gloves za wakia nane (8 oz) zitatumika kwa mapambano ya mabondia wenye uzito usiozidi na mpaka kgm 67 Na gloves za wakia kumi (10 oz) kwa mabondia wenye kuzidi uzito wa kgs 67.

 

Afya:



7       Ni lazima bondia apimwe afya siku ya pambano kabla hajaingia ulingoni kushindana.

Vifaa vya Usalama:

8       Wakati wa pambano, ni lazima bondia avae kinga za mbeleni ( Protector cap) kabla ya kuvaa kaptura ya michezo.

9       Wakati wa pambano, ni lazima bondia avae kinga ya meno (Gumshield).

10    Kabla ya kuvaa gloves ni lazima bondia avae bandeji.

11    Viatu visivyo na visigino.

12    Ni lazima avae kaptura ya michezo isiyozidi mwisho wa magoti

Urefu wa Raundi ya Pambano:

13    Kila raundi ya pambano la ngumi za wanaume litakuwa ni dakika tatu (3) za kupigana zikiwa na mapumziko ya dakika moja (1) kati ya raundi na raundi.

14    Kila raundi ya pambano la ngumi za wanawake litakuwa ni dakika mbili (2) za kupigana zikiwa na mapumziko ya dakika moja (1) kati ya raundi na raundi.

15    Hakuna pambano lolote lile litakalopiganwa chini ya raundi nne (4) na kutambuliwa kama shindano.

16    Hakuna pambano lolote lile litakalopiganwa zaidi ya raundi kumi na mbili (12)

17    Pambano la ubingwa wa Tanzania litakuwa ni la raundi kumi (10) tu.

18    Hakuna pambano ambalo la ushindani ambalo litapiganwa kwa raundi zisizoganyika kwa mbili (2). Yaani kutakuwa na mapambano ya raundi nne (4), raundi sita (6), raundi nane (8), raundi kumi (10) na raundi kumi na mbili (12).

Muundo na jumla ya waamuzi wa pambano:

19    Mapambano yanaweza kuamuliwa na refa bila msaada ya waamuzi wengine.

20    Mapambano mengine ni lazima yawe na watu watatu (3) wanaotoa pointi.

21    Refa anaweza kutoa pointi akisaidiwa na waamuzi wawili (2) AU refa asitoe pointi bali awe na waamuzi watatu (3) wa kutoa pointi.

Wasifu wa refa anayechezesha pambano:

22    Jukumu kuu la refa ni kulinda usalama wa mabondia na kutunza heshima ya mchezo wa boxing kwa kuhakikisha kuwa sheria zinafuatwa.

23    Ni refa pekee ndiye mamlaka ya mwisho juu ya mwenendo wa pambano ndani ulingo. Aidha ni refa tu ndiye aliye na mamlaka ya kusimamisha pambano.

24    Ni refa pekee ndiye mwenye mamlaka ya kuamua iwapo tukio ni bahati mbaya au ni kusudio.

25    Ni wajibu wa refa kusimamisha pambano iwapo bondia ataumia kiasi cha kuharibu maana nzima ya boxing kama mchezo. Hata hivyo ni vizuri refa atafute maoni ya daktari wa pambano.

26    Kuvuja damu kutokana na kuchanika juu ya jicho ni moja ya sababu ambazo zinamruhusu refa kusimamisha pambano.

27    Refa ataheshimu na hatakiwi kuupinga uamuzi wa marefa wengine wa pambano (judges) au kamisaa wa pambano inapotokea utata.

28    Ni wajibu wa refa kuhakikisha kuwa hakuna bondia anaanza raundi ya kupigana bila kuwa na gumshield.

29    Ni wajibu wa refa kumhesabia mpinzani aliyeangushwa chini na kipigo halali.

Kusimamisha pambano kwa ajili ya usalama wa mpiganaji:

30    Bondia anapohisi amezidiwa na kipigo cha mpinzani anaweza kusimamisha pambano kwa kuinua mikono juu au kwa kumuarifu refa.

31    Msaidizi wa bondia anaweza kusimamisha pambano kumwokoa bondia wake asiendelee kupata kipigo kwa kutupia taulo ndani ya ulingo.

32    Ni wajibu wa refa kusimamisha pambano ili kumwokoa bondia asiumie kwa kuendelea kupata kipigo baada ya kuzidiwa na mpinzani.
Mtindo wa kutoa pointi za boxing :

33    Kila mshindi wa raundi atapata pointi kumi (10 points system) na atakayeshindwa atapata pungufu ya pointi lakini siyo chini ya pointi 7 kwa raundi.

34    Kufanyika kwa faulo kunaweza kufanya bondia apewe onyo na refa au kutolewa pointi au kushindwa kwa disqualification.

35    Kila mwamuzi (judge) anayo ruhusa ya kumpunguza pointi kwa mpiganaji anayefanya faulo bila kungojea onyo la refa.

Faulo za msingi katika boxing:

36    Hairuhusiwi kupiga mgongoni wala kisogoni.

37    Hairuhusiwi kupiga sehemu ya kinena.

38    Hairuhisiwi kupiga kwa kutumia kichwa.

39    Hairuhusiwi kumpiga mpinzani aliyeanguka chini. Mpinzani atahesabiwa kuwa ameanguka chini iwapo sehemu yoyote ile zaidi ya nyayo itagusa turubai la ulingo.

40    Hairuhusiwi kupiga ngumi za kelebu wala makofi.

41    Hairuhusiwi kupiga baada ya kengele ya kuashiria kuisha kwa raundi.

42    Hairuhusiwi kutumia lugha ya matusi.

43    Hairuhusiwi kujiangusha bila ya kupigwa.

44    Hairuhusiwi kutia kabali wakati wa kipiga au kupigwa.

45    Hairuhusiwi kupiga iwapo refa atasema STOP.

46    Kukimbia kwa woga ulingoni kukwepa mpambano.

Kushindwa kwa Disqualification:

47    Bondia akimuumiza mpinzani kwa faulo kiasi refa kulazimika kusimamisha pambano, basi bondia huyo atashindwa pambano kwa disqualification.

48    Kitendo cha kupigwa kwenye kinena si sababu ya msingi ya kupata ushindi kutokana na disqualification.

49    Uamuzi wa kutoa ushindi kwa disqualification uko mikononi mwa refa tu.

Knockdown, knockout (KO) na Technical knockout (TKO):

50    Bondia atafahamika kuwa ameangushwa chini iwapo atagusa canvas ya ulingo kwa sehemu nyingine yoyote ya mwili wake zaidi ya nyayo au amesimama wima kwa kuwa tu amegemea au ameushika ulingo.

51     Bondia atakayeangushwa chini kutokana na kupigwa pigo halali atafahamika kuwa amepigwa knockdown na atahesabiwa nukta nane ( 8 mandatory count) na atakatwa pointi moja (1) au mbili (2).

52    Bondia atakayeangushwa nje ya ulingo kutokana na kupigwa pigo halali atafahamika kuwa amepigwa knockdown na atahesabiwa nukta ishirini ( 20 mandatory count) na atalazimika kurudi ulingoni bila msaada wa mtu yeyote atakatwa pointi moja (1) au mbili (2).

53    Bondia atakayeonyesha kupoteza fahamu baada ya kupigwa pigo halali atahesabiwa nukta nane ( 8 standing count) na atakatwa pointi moja (1).

54    Bondia akishindwa kuamka kuendelea baada ya kuhesabiwa hesabu yoyote ya lazima (mandatory count) baada ya kuangushwa chini ( knockdown) basi atakuwa ameshindwa pambano kwa Knock Out.

55    Bondia akijiuzulu au msaidizi wake akitupia taulo ulingoni au msaidizi wa bondia akimwomba refa asimamishe pambano ili bondia wake asipate kipigo zaidi, bondia atakuwa ameshindwa kwa TKO.

56    Refa akisimamisha pambano kumwokoa bondia basi bondia huyo takuwa
          ameshindwa kwa TKO.

57    Kuangushwa chini (knockdown) mara tatu (3) katika raundi kutokana na kipigo kichwani ni kushindwa wa Knock Out moja kwa moja.

58    Hata hivyo refa anaruhusa ya kumhesabia bondia kutokana na pigo lolote lile halali litakalomfanya bondia apoteze fahamu.



Pambano litakalosimishwa kutokana na pigo batili (Kichwa).

59    Pambano lolote litakalosimamishwa kutokana na mpinzani mmoja kuumia juu ya jicho kwa kupigwa kichwa kwa bahati mbaya, basi mshindi ni yule aliyekuwa akiongoza kwa pointi iwapo pambano lilikuwa limevuka raundi tatu (3).

Kama pambano litakuwa halijavuka raundi tatu (3) basi litahesabiwa ni sare ya kiufundi (Technical Draw).

60    Pambano lolote litakalosimamishwa raundi yoyote ile kutokana na mpinzani mmoja kuumia juu ya jicho kwa kupigwa kichwa kwa kusudio, basi mshindi ni bondia aliyepigwa kichwa.

61    Ni refa pekee ndiye mwenye uamuzi kuhusu pigo la kichwa kuitwa ni bahati mbaya au kusudio.

Pigo chini ya mkanda (Kinena).

62    Pigo la kusudio kwenye kinena litamfanya mpigaji apototeze pointi moja (1) iwapo pigo la namna hii ni rudio.

63    Pigo la kusudio kwenye kinena halimpi ushindi wa disqualification mtu aliyepigwa bali refa ana mamlaka ya kutoa pumziko lisilozidi dakika tano (5) kwa mtu aliyepigwa ili aweze kupata ahueni. Akikataa kuendelea basi atashindwa kwa TKO.

Pambano litakalosimishwa kutokana na sababu nyingine.

64    Pambano likisimamishwa kutokana na giza ndani ya ulingo au fujo ya watazamaji au sababu nyingine ambazo ziko nje ya uwezo wa binadamu basi pambano hilo halitakuwa na mshindi (No contest).

                                        ---------Mwisho-----