Adverts

Feb 23, 2013

HALI YA BARABARA TUNDUMA -SUMBAWANGA TETE



 HAPA BASI LA SUMRY LINATANGA NA NJIA! HAKUNA PA KWENDA BAADA YA KUKWAMA KWENYE MATOPE HUKU MZUNGU ANAPIGA SIMU BAADA KUITA MSAADA BAADA YA GARI LAKE KUTUMBUKIA WAKATI LIKITAKA KUPITA PEMBENI MWA BASI LA SUMRY KIJIJI CHA MENGO
 HII NI KAWAIDA KUTOKA TUNDUMA KWENDA SUMBAWANGA-BARABARA UJI UJI
 MAOFISA WA HALMASHAURI YA WILAYA YA MOMBA WAKIWA WAMETOA MACHO BAADA YA MSAFARA WAO KUZUIWA NA KUKWAMA KWA BASI LA SUMRY PAMOJA NA ROLI LILILOKUWA LIKIELEKEA SUMBWAWANGA
 ZANA HIZI AMBAZO NI ZA UKWAMUAJI ZIKIENDELEA KUDUNDA MZIGO MPAKA ZIPEWE AMRI NA BOSI!!KWENDA KUONDOA MATOPE KWENYE DIVERSIONS
 MAFUNDI WA UJENZI WAKIENDELEA KUTENGENEZA KARAVATI KATIKA BARABARA HIYO
HATIMAYE MTAMBO SASA UMESOGEA KUWEKA SAWA BARABARA IANZE KUPITIKA 
PICHA ZOTE NA GODFREY MWAKITWANGE WA INDABAAFRICA BLOGSPOT

Na Danny Tweve wa indabablogspot Tunduma

Abiria wanaosafiri kati ya Mbeya na Sumbawanga wameomba serikali kutoa maelekezo kwa kampuni zinazojenga barabara hiyo kuweka utaratibu wa  kuyakwamua magari yanayokwama kwenye barabara za muda zinazojengwa kuchepusha maeneo ya mradi hasa wakati huu wa mvua na matope

Wakizungumza kwenye kijiji cha Mengo katika Tarafa ya Ndalambo, abiria waliokuwa wakisafiri na basi la Sumry kutoka Mbeya kwenda Sumbawanga wamesema, kampuni hizo zimekuwa hazitoi ushirikiano na badala yake kuyatelekeza magari yanayokwama kwenye eneo la miradi yao  huku wao wakiendelea na ujenzi kando mwa maeneo ambamo mabasi yamekwama

Abiria hao Tacisius Shoo, Bi Neema Msongole na Bi Mariam Kalegea  wamesema hali ya barabara hiyo kwa sasa inahitaji uangalizi wa karibu hasa kwenye maeneo ambayo kampuni za ujenzi zimechepusha barabara hizo na kwama imekuwa hali ya kawaida kwa abiria kushinda kutwa nzima wakisubiria matope yakauke ndipo waendelee na safari

Akizungumza kwenye eneo hilo mmoja wa wakalimani wa wasimamizi wa barabara hiyo ambaye hakujitambulisha jina lake alisema, wamekuwa na utaratibu wa kuyakwamua magari yanayokwama kwenye maeneo yao ya mradi na kwamba kuchelewa kwa basi la sumry kumetokana na opareta wa chombo cha kusafisha barabara kutoka kidogo

Juzi ujumbe wa viongozi wa wilaya ya Mbozi na Momba waliokuwa wakienda kuangalia chanzo cha mradi mpya wa  Uzalishaji umeme unaokusudiwa kujengwa kijiji  cha Mfuto wilayani Momba, walishuhudia hali hiyo baada ya kampuni ya Consolidated Construction Company (CCC) kuchepusha barabara kijiji cha Mengo na barabara hiyo kutitia kutokana na hali ya mvua inayoendelea kunyesha.

Hata hivyo baada ya majadiliano ya muda na viongozi  wa wilaya na msimamizi wa eneo la mradi, kampuni ilitoa mashine moja kwenda kusafisha eneo korofi la barabara hiyo  na kuruhusu mabasi yaliyokuwa yamekwama kwa zaidi ya masaa matatu kuendelea na safari

Mmoja wa maafisa wa kampuni hiyo licha ya kutoa ushirikiano kwa kusimamia usafishaji wa eneo hilo ili magari yaliyokwama yaendelee na safari alisema siyo msemaji wa kampuni na kwamba wamejiwekea utaratibu wa kuyakwamua magari yanayokwama kila baada ya muda wa masaa matatu kila siku ili kuwezesha na shughuli za mradi kuendelea.

Mwisho