Adverts

Jul 3, 2024

SASA YANAPATIKANA VWAWA MKOA WA SONGWE

 MAGARI YA WATOTO 



SASA BLOG KUTUMIKA KUSAMBAZA BIDHAA

 Indaba africa sasa itakuwa uwanja wa biashara kwa wauzaji na wanunuzi kukutana,lengo ni kuongeza uwigo kwa wajasiliamali kupata masoko na kukutanishwa na wanunuzi hivyo Digital platform kuwa eneo muhimu la kukuza uchumi. 

Sep 12, 2018

FAIDA ZA MAJI YA DAFU

Maji ya Nazi ni kinywaji  kinachojitokeza ndani ya nazi mbichi almaarufu kama dafu ambayo huwa rangi ya  kijani. Maji hayo huwa na kiwango cha mafuta 0, cholesterol 0 na ni chini ya kalori. Faida kuu ya maji ya nazi ni kwamba  maji haya yana kiwango kikubwa cha  electrolytes kuzalisha  kiwango cha upozaji mwili kwa siku nzima katika mazingira ya joto hata baada ya kuyanywa kwa muda mrefu  hadi usiku wakati mwingine huendelea kupoza mwili.

Maji ya dafu  yana madini ya Potasium  zaidi kuliko ndizi, na mara 15 kiasi kinachopatikana katika vinywaji vya asili vingine. Potasiamu husaidia kuzuia kunywea kwa  misuli.

Baadhi ya makampuni ya maji ya nazi huongeza juisi kwa ladha ya bidhaa zao, ambazo zinaweza kusababisha sukari nyingi na kalori, hivyo utahitaji kuepuka hilo, lakini maji safi ya nazi ni mbadala nzuri ya vinywaji vinavyoweza kutumika  michezoni  badala ya matumizi ya vinywaji  bandia ama vya viwandani  na vinywaji vingine vya sukari.

Jun 4, 2018

BENKI YA NMB YAJIELEKEZA KUJENGA UWEZO KWA VIKUNDI

Benki ya NMB Tawi la Mbozi na Mlowo kwa pamoja wameelezea nia yao ya kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Mbozi katika kushughulikia changamoto za ukuaji na uaminifu kwa vikundi vya wakulima ili mikopo inayopatikana iwe na tija kiuchumi 
Wakizungumza na menejimenti na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi, Timu ya wataalamu wa benki hiyo wamesema bado jamii ya wananchi wa Mbozi hawajafikiwa vyema na elimu ya Mikopo kiwango ambacho wengi wa wanaojitokeza kukopa  kutokujipanga vyema kulingana na mipango yao.
Wamesema ikiwa halmashauri inaona vyema kutoa huduma zake kupitia vikundi ni vyema wakaishirikisha benki hiyo ili kujenga uwezo na kuandaa wajasiliamali wenye nia ya dhati  ya kujikwamua na umaskini kwanza badala ya kuanzisha programu za hamasa juu ya mikopo mbalimbali bila kuwaandaa kwanza 

VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA VINGI VYAVUKA KIKWAZO KWENYE VIGEZO 2017/2018

Vituo vya kutolea huduma za afya 19 tu kati ya 80 ndivyo vilivyopata nyota sifuri katika tathmini ya mwaka 2017/2018 imefahamishwa.
Wakitoa taarifa ya ukaguzi wa  hali ya vituo hivyo kwa kuzingatia mwongozo wa BRN, Wakaguzi wa wizara ya Afya wamesema kuna ongezeko kubwa la vituo vilivyovuka kutoka nyota sifuri hadi kuingia kwenye nyota moja ikilinganishwa na mwaka 2016.
Kwa mwaka 2016 vituo 45 vilipata nyota 0 kati yake vikiwemo zahanati 45 lakini kwa mwaka huu hali imekuwa tofauti ambapo Zahanati 19 kati yake 16 za serikali zimepata nyota sifuri, zahanati  48 zimepata nyota moja, 8 Nyota Mbili ambapo vimo vituo vya afya na Hospitali ya Misheini ya Mbozi na  Hospitali ya wilaya ya Mbozi imepata Nyota tatu.
Katika mchanganuo huo Zahanati ya Mbaya ambayo ni Binafsi imeshika nafasi ya mwisho kwa kupata wastani wa alama 0.
Katika uchambuzi huo miongoni mwa mapungufu yaliyobainishwa nipamoja na  vituo 63 kati ya 80 kutokuwa na vyoo seti tatu kama mwongozo unavyotaka ambapo inashauriwa kuwa na vyoo vya wanawake, wanaume na watoa huduma (wataalamu) kwenye majengo ya zahanati, aidha kukosekana kwa vyoo rafiki kwaajili ya walemavu na wenye mahitaji maalumu.
Katika ukaguzi huo kulikuwa na jumla ya Maeneo 12 yaliyowekwa kwenye makundi katika ukaguzi yakiangalia uwezo na uendeshaji wa vituo vyenyewe ikiwa ni pamoja na miundombinu yake, utendaji wa wataalamu, Matumizi ya zana, vitendanishi na takwimu za afya zilizopo kituoni katika kupanga mipango ya mbele, ushughulikiaji wa  huduma za dharura, mtazamo wa kumlenga mteja na uwajibikaji.

HALMASHAURI YA WILAYA YA MBOZI YAJIELEKEZA KUFIKIA 100% YA MAKUSANYO

Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi imeagizwa kusimamia ukusanyaji wa mapato yake ya ndani kwa asilimia 100, ili iweze kutekeleza miradi yake iliyopangwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi akiwa na wajumbe wenzake wa kamati ya Fedha ya Halmashauri hiyo ametoa msimamo wa madiwani wakati akizungumza na wananchi kata ya Isansa baada ya kamati hiyo kujiridhisha na ujenzi wa kituo cha afya unaofanywa kwa njia ya Force account.
Amesema wakati zimesalia siku chache kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2017/2018 ni vyema wataalamu wakatambua kuwa Halmashauri ya wilaya haijafanikiwa kutekeleza baadhi ya miradi ya Maendeleo kutokana na mapato kidogo ya ndani ambapo hadi kufikia Juni Mosi Halmashauri imefikia asilimia 78 ya makusanyo yake ya ndani hata hivyo kuna vyanzo vingi zikiwemo leseni za biashara ambazo bado hazijaweza kukusanywa vyema, hivyo mkakati wake kwa sasa ni kujielekeza kukusanya kwenye vyanzo hivyo sambamba na mazao baada ya msimu wa mavuno kuanza.
Kutokana na hatua hizo tayari timu ya mapato ya Halmashauri ya wilaya ya Mbozi imeundwa ikihusisha wataalamu wa idara mbalimbali, huku kamati ya fedha ya Halmashauri hiyo ikikasimiwa majukumu ya kusimamia utendaji wa menejimenti katika kipindi chote ili kuhakikisha kuwa malengo yanafikiwa.
Kwa upande wao wataalamu wameahidi kutekeleza wajibu wao hasa katika suala la makusanyo na kwamba matarajio yao ni kuona kuwa Halmashauri yao inafanya vyema katika utekelezaji wa malengo yake ikiwemo miradi iliyopangwa.

May 29, 2018

DAWA YA KINGA YA VVU KULENGA MAKUNDI MAALUM

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo Mfuko wa Henry Jackson kutoka serikali ya Marekani wamo kwenye hatua za maandalizi kwaajili ya kutekeleza mpango wa utoaji dawa kinga kwa watu walio katika makundi maalumu ya jamii ambayo yapo kwenye hatari ya kuambukizwa.
Kulingana na taarifa za utekelezaji wa Mpango huo, wanawake wanaouza ngono pamoja na wanaume walio kwenye biashara hiyo watashiriki kwenye mpango huo baada ya hatua za awali ambapo watahamasishwa kujipima wenyewe na ikithibitika wana maambukizi wataunganishwa na huduma za CTC ikiwa ni pamoja na kuingizwa kwenye mpango wa matumizi ya dawa za kupunguza makali ARV's
Ama kwa upande mwingine wale ambao hawatakutwa na maambukizi, wataanza kutumia dawa kinga ambapo kila siku watawajibika kumeza kidonge kimoja kwa kipindi kinachofikia siku 21 mfululizo huku pia wakitumia njia za kinga zingine zinazoelekezwa kitaalamu. Hatua hiyo inalenga kupunguza uwezekano wa mtumiaji wa dawa kinga kuambukizwa na virusi ikiwa ataacha kutumia njia zingine ikiwemo matumizi ya Kondomu katika kipindi cha matazamio ya dawa.
Kutokana na takwimu kuonyesha nchini Tanzania asilimia 25 ya wanawake wanaouza ngono wamo kwenye hatari ya maambukizi na katika utafiti uliofanyika hivi karibuni walibainika kuwa na maambukizi ya VVU, wakati ambapo 26% wanaume wanaofanya ngono ya wanaume kwa wanaume pia walibainika kuwa na maambukizi wakati 36% ya wanaotumia dawa za kulevya pia walikutwa na maambukizi hayo.
Mpango huo utatekelezwa kwenye vituo vya afya vyenye huduma za CTC,kwa kuzingatia idadi ya wateja wanaotumia ARV's, Uwepo wa wataalamu waliopata mafunzo ya utoaji huduma kwa watu wanaoishi na VVU.
Kutokana na utaratibu huo si kila Mtanzania atafikiwa na Dawa Kinga hiyo hivyo imesisitizwa umuhimu wa watanzania kuendelea kutumia njia za kinga zilizoelekezwa na wataalamu ili hatua ya majaribio ya dawa Kinga ya sasa yaweze kupimwa kwenye kundi lengwa la wanaouza ngono kwa baadhi ya maeneo yaliyoingizwa kwenye mpango huo katika Mkoa wa Mbeya na Songwe.

UMISETA MOTO- SONGWE YAKOLEZA JIKO KUTETEA UBINGWA TAIFA

Timu ya Umoja wa wanafunzi wa Sekondari  -Mkoa wa Songwe, imo kwenye hatua za mwisho kwenda kushiriki mashindano ya Taifa yanayokusudiwa kufanyika Mkoani Mwanza. Timu hiyo imeundwa rasmi na orodha ya wachezaji kusomwa mbele ya afisa elimu Mkoa wa Songwe JUMA MHINA juzi katika uwanja waa shule ya sekondari ya Vwawa.
Timu hiyo yenye wachezaji 120 itawakilisha mkoa wa Songwe katika michezo ya Mpira wa Miguu kwa wanaume, Mpira wa Pete, Riadha, Mpira wa mikono, Mpira wa Kikapu na michezo ya ndani.Mkoa wa Songwe ndiyo bingwa wa taifa ka mwaka uliopita ambapo iliweza kuwadungua Unguja kwenye mpira wa Miguu katika fainali.

Jul 22, 2016

MKUU WA WILAYA YA MBOZI AWATAKA MADIWANI KUWAFUATILIA WALENGWA WA TASAF



Mkuu wa wilaya ya Mbozi Bw. John Palingo amewataka madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi kufanya ufuatiliaji kwa walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa chini ya TASAF awamu ya tatu.

Akitoa salamu za serikali, Mkuu wa wilaya ya Mbozi amesema kuwa hatua hiyo itawarudisha kwenye mstari walengwa kutokana na kuwepo taarifa za matumizi mabaya ya fedha wanazonufaika kupitia mpango huo

Katika hatua hiyo amesisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kutekeleza azma ya mpango huo kufikiwa .

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya ametangaza nia ya kurejesha na kuzifungua barabara za katikati ya mji wa Vwawa  na kwamba kitaitishwa kikao cha wadau wa maendeleo mji wa Vwawa ili kujadili jambo hilo mchana wa leo ama kesho asubuhi ili hatimaye kufikia maamuzi ya pamoja ya namna bora ya uendelezaji wa huduma ya usafiri na uchukuzi mjini.

Polisi Songwe yaja na Ligi ya vijana msimu wa mavuno


Jeshi la Polisi kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo wilayani Mbozi katika mkoa wa Songwe  wanakusudia kuanzisha ligi ya vijana itakayoanza kulindima mwezi August, 2016

Akizungumza na mtandao huu, Mkuu wa polisi wilaya ya Mbozi Henry Kyssima amesema hatua hiyo inalenga kubaini vipaji vya vijana na hatimaye kutumia ligi hizo kuwaunganisha na timu mbalimbali zinazoanza ligi hivi karibuni

Ligi zinazokusudiwa kuwavizia wachezaji hao ni pamoja na zile za ligi kuu, daraja la kwanza na daraja la pili ambazo tayari kufuatia mwaliko huo kuna ugeni mkubwa ambao umeanza kuvinjali katika wilaya ya Mbozi na vitongoji vyake kwaajili ya kusaka vipaji hivyo

Kyssima amesema anatambua kuwa kipindi cha August kuna shughuli nyingi za kiuchumi zinazoendelea wilayani hivyo katika kuendesha ligi hiyo, itasaidia pia kutumia muda wa mapumziko katika michezo badala ya kuelekeza fedha na mapato yao kwenye matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu

Amesema ligi hiyo itaendeshwa kwenye kanda tano na baadaye washindi wa kanda watakutanishwa hadi kupatikana kwa mshindi wa wilaya.

Jan 21, 2016

UTOAJI WA CHAKULA MASHULENI BADO CHANGAMOTO

Baraza la Madiwani wilaya ya Mbozi leo limeelezwa kuwa suala la utoaji wa chakula shuleni, bado limeendelea kukwaza mafanikio ya utendaji na ufaulu wa watoto kwenye shule za msingi.

Hayo yamejitokeza wakati wa kikao cha baraza la madiwani kupitia taarifa za kata ambapo imebainika kuwa shule nyingi ambazo hazikufanya vizuri kwenye matokeo ya darasa la saba ni zile ambazo hazina mpango wa chakula.

Shule ya Izyaniche ambayo mwaka juzi iliongoza kiwilaya katika miaka miwili mfululizo imekuwa ya mwisho kiwilaya na ni miongoni mwa shule 10 kimkoa za mwisho


Jan 8, 2016

SAMMATA AIPAISHA TANZANIA ,ANYAKUA TUZO

Hatimaye Mbwana Ally Sammatta ameiwakilisha vyema Tanzania baada ya kushinda miongoni mwa wachezaji wazawa wa Afrika kama mchezaji bora wa Mwaka anayechezea ligi za ndani ya Afrika
 Samatta anaungana na Mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang kutoka Gabon kuwa vinara wa CAF kama wachezaji bora wa mwaka 2015 kwa mara ya kwanza.

Samatta anakuwa mchezaji wa kwanza ukanda wa Afrika Mashariki kutwaa tuzo hiyo akiwa mchezaji bora anayeshiriki ligi za ndani barani Afrika

Mbwana Samatta amewafunika wenzake akiwemo mchezaji mwenzie wa Tp Mazembe  na kipa wa DRC CONGO Robert Muteba Kidiaba ambaye aliinuka na pointi 88, na kufuatiliwa na mchezaji kutoka Lgeria Baghdad Bouneydjah aliyepata pointi 63
 Wakati utamu huo ukimjia Samatta na taifa lake Tanzania, Majonzi yamehamia kwa wachezaji wakongwe akiwemo Yaya Toure kutoka Ivorycost na Ayew Andre wa Ghana ambao wamenyanyasika mbele ya mchezaji kinda wa miaka 26 Aubameyang aliyezoa pointi 143 zikiwa saba zaidi ya alizopata Toure huku Ayew akipata 112
 chanzo vanguard








Jan 6, 2016

MADIWANI MBOZI WAPIGWA DARASA MBOZI

Madiwani wapya wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi kwa mfululizo wa siku mbili wamehudhulia mafunzo ya kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao.
 Miongoni wa taasisi zilizoshiriki kuwajengea uwezo ni pamoja na Ofisi ya kanda ya maadili ya utumishi wa Umma, Ofisi ya katibu tawala mkoa na wakuu wa idara za halmashauri ya wilaya.Eneo pekee lililozua maswali mengi ni suala la maadili ya utumishi wa umma, mahusiano baina ya serikali kuu na serikali za mitaa ambapo masuala ya mwingiliano wa kiutendaji na masuala ya ufuatiliaji maadili ya watumishi yalijadiliwa kwa upana.


Jan 5, 2016

REA WAPOKELEWA VIJIJINI KWA SAHANGWE LAKINI....

Wakazi wa kata ya Kigala wamepongeza hatua ya wakala wa Umeme vijijini REA kutekeleza mpango wa usambazaji wa umeme katika kijiji kimoja cha kata hiyo, hata hivyo wameonyesha hofu yao kutokana na mradi huo kuonyesha dalili za kuishia kijiji kimoja!Ingawa hakuna maelezo ya kitaalamu juu ya sababu za mradi huo kusimama licha ya kazi ya survey kufanywa hadi kijiji cha Kigala,ni kijiji cha Mlengu pekee ambacho mradi huo umeshatekelezwa na mkandarasi anaonekana kumalizia usambazaji kwenye kijiji hicho pekee.Hali hiyo imemsukuma mheshimiwa Diwani wa kata hiyo Nguvila kuanza kufuatilia ngazi za juu kutokana na kuelezwa kuwa mkandarasi wa mradi wa kupeleka umeme kijiji cha Kigala ni mwingine.Kwa ujumla jitihada za kuunganisha umeme vijiji vya kata ya Ikuwo na Kigala katika wilaya ya Makete zimepokelewa kwa mikono miwili na wananchi wa maeneo hayo na kupongeza jitihada za mbunge wao aliyemaliza muda wake Dr Binirith Mahenge ambaye aliasisi mchakato huo na kuusimamia. Wanaeleza kuwa matarajio yao ni kuona kuwa Mbunge wa sasa Mh Dr Norman Sigala anatoa msukumo zaidi katika kuhakikisha vijiji vilivyopangwa kutekelezewa mradi huo vinanufaika.Kwa mazingira ya vijiji hivyo kupata umeme wanaona ni sawa ya ndoto ya mchana kwakuwa tangu uhuru wamekuwa wakihangaika na miundombinu hasa barabara na hawakutegemea suala la umeme hivyo hatua ya sasa ni dalili ya ukombozi kiuchumi kwa wananchi hao na kwamba kutachangia uanzishaji wa viwanda vingi vijijini.








Msimu wa upandaji miti Mkoa wa Njombe waanza

Wakazi wa mkoa wa Njombe wameanza msimu mpya wa upandaji miti ambapo shughuli hizo sasa zimepewa umuhimu mkubwa tofauti na hapo nyuma ambapo programu mbalimbali za uhifadhi mazingira zilitekelezwa na kuhamasisha wananchi bila mwitikio mzuri.
Katika vijiji vya Kigala, Mlengu, Ikuwo,Matenga na Nkondo,wananchi wamejiwekezea akiba zao kwenye upandaji miti ambapo sasa angalau kila kaya ina angalau ekari moja ya miti hali inayoashiria kuwa miaka michache ijayo kutakuwa na mabadiliko makubwa.
Tishio lililopo kwa sasa ni kuwepo kwa taarifa kuwa Pori la akiba la Mpanga -Kipengere linakusudiwa kupanuliwa hivyo kuvifuta baadhi ya vijiji, hali hii inapunguza ari ya wananchi kupanda miti kwa kasi katika maeneo yao licha ya kupokea vyema mpango wa upandaji miti.Mzee Mafundihano Nzilani pichani anaeleza kuwa amejijengea utamaduni wa kupanda miche 100 kila mwaka na kwamba tayari keshaanza kufaidi matunda ya miti aliyoipanda miaka 15 iliyopita.






TUMERUDI TDNA

Mtandao wa indaba africa umerejea tena baada ya kuwa nje ya mawasiliano na jamii kwa muda mrefu. Hii ilitokana na mwendeshaji kukabiliwa na majukumu yaliyomfanya ashindwe kuusimamia.kwa sasa wasomaji wataendelea kupata habari humu

Jul 3, 2015

STARZ KUTUTOA MATONGO TONGO KESHO



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI - RELEASE NO. 111
TAREHE 03 JULAI 2015


STARS KUWAVAA THE CRANES KESHO
Taifa Stars inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premieum Lager kesho jumamosi saa 10 kamili kwa saa za Afrika Mashariki itashuka dimba la Nakivubo kucheza na wenyeji Uganda.(The Cranes).

Mecho hiyo ya kesho ni mchez wa marudiano kuwania kufuzu kwa fainali za CHAN mwaka 2016 zitakazofanyika mapema mwezi Januari nchini Rwanda, mgeni rasmi atakua Rais wa Uganda Yoweri Mseveni.

Kikosi cha Taifa Stars chini ya kocha wake mkuu Charles Mkwasa, kiliwasili jijini Kampala jana usiku na kimefikia katika hoteli ya Grand Global iliyopo jirani na chuo kikuu cha Uganda Makerere.

Taifa Stars imefanya mazoezi leo jioni katika uwanja wa Nakivubo yakiwa ni mazoezi mepesi na mwisho kuzoea uwanja kabla ya mchezo wenyewe utakaofnayika kesho jioni.

Kocha Mkwasa akiongelea kuelekea mchezo huo amesema, anashukuru vijana wake wamefika salama wote, hali nzao ni nzuri, morali ni ya hali ya juu, kikubwa wanatambua wana deni kubwa kwa watanzania hivyo kesho watapambana kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

Akiongelea hali ya hewa na mazingira ya timu ilipofikia, Mkwasa amesema hali ya hewa ni ya kawaida baridi na mvua kidogo haina tofauti sana na Tanzania, mazingira ya hoteli ni mazuri na kusema kikubwa kilichobaki ni kusaka ushindi katika mchezo huo na vijana wake wapo tayari. 

Wakati huo huo mashabiki zaidi ya 50 kutoka nchini Tanzania wanatarajiwa kuwasili kesho jumamosi alfajiri wakitokea jijini Dar es salaam kuungana na watanzania wengine waishio nchini Uganda kuishangilia timu ya Tanzania itakapokuwa ikipimbana na Uganda katika uwanja wa Nakivubo.

Mawasiliano ya Afisa Habari wa TFF aliyepo Uganda ni +256 780 177008

NB: picha za mazoezi ya Taifa Stars Nakivubo leo zimeambatanishwa

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

KIMONDO YAAMUA KUMWAGA MBOGA, YAWEKA HADHARANI MIKATABA YA MWASHIUYA



Kimondo Super Sports Club
P.o Box 30, Mbozi.Mob.0755708828, 0764947555 E-mail:  kissc@gmail.com
OUR REF NO: KISSC/GC/02/07                                            03/07/2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KIMONDO BADO INATAMBUA KUWA GEOFREY B.MWASHIUYA NI MCHEZAJI WAKE MPAKA MSIMU WA 2017/2018
Klabu ya Kimondo Super Sports inayoshiriki ligi daraja la kwanza Tanzania yenye maskani yake wilayani Mbozi inapenda kutoa tamko juu ya mkanganganyiko wa taarifa za kuptosha za usajili wa mchezaji wake Geofrey Bahati Mwashiuya.
Klabu inasikitishwa saana na habari/taarifa zenye mkanganyiko zinazotolewa na msemaji wa timu ya Yanga,Katibu wa timu ya Yanga na mchezaji wetu Geofrey Mwashiuya katika vyombo mbalimbali vya habari;
Jerry Muro alisikika katika vyombo vya habari akijinadi kuwa klabu ya soka ya Yanga imemsajili Geofrey Mwashiuya tangu Oktoba,2014 kwa kandarasi ya miaka mitatu,wakati huohuo Katibu wa Yanga Dkt,Jonas Tiboroha alidai mchezaji huyu alisajiliwa na klabu ya Yanga tangu mwezi Februari,2015.
Klabu ya KIMONDO inasikitishwa na taarifa hizi zenye mkanganyiko mkubwa kuhusu suala la mchezaji huyu,na kwa kauli hizo mbili zinazokinzana Watanzania wanaweza kuona ukweli wa mambo ukoje.
Taarifa sahihi ni kwamba mchezaji Geofrey Mwashiuya ana mkataba wa miaka minne na timu yetu ya KIMONDO  na ndio muda sahihi ulioandikwa katika TMS na uliopo katika mkataba wa maandishi. Zaidi klabu ya KIMONDO inasikitishwa na taarifa hizi za upotoshwaji zinazofanywa na YANGA kwa makusudi kabisa kuwa mchezaji wetu hana mkataba na sisi,
Pia maneno ya mchezaji akijaribu kuudanganya umma wa Watanzania na wapenda soka kuwa alipewa kijikaratasi tu cha kujaza,alipokwenda TFF na Uongozi wa YANGA wakaarifiwa kuwa hiyo ni fomu ya uthibitisho wa mchezaji. Zaidi wanadai kuwa TFF iliwaambia kuwa mchezaji wa daraja la kwanza mara ifikapo mwisho wa msimu/ligi basi na mkataba wa mchezaji unakuwa umekwisha.
 Pia klabu ya KIMONDO ilisikia maneno hayo yaliyotamkwa na mchezaji yakiungwa mkono na katibu wa YANGA katika kipindi cha michezo cha anga la michezo cha Ebony Fm na mitandao ya kijamii siku ya jumatatu tarehe 29,June,2015 akijinasibu kuwa kwa uelewa wake ligi daraja la kwanza haina mikataba na mchezaji huwa huru mara ligi inapomalizika.Kwa msingi huo wanatambua kuwa ligi daraja la kwanza wachezaji wake wanakuwa na mikataba ,kama sivyo ni sababu zipi zilizowapelekea wao kudai kutuandikia barua sisi ya kutaka ufafanuzi wa mikataba ya wachezaji wetu na zaidi kwenda TFF?
 Klabu ya KIMONDO inahoji juu ya utaratibu huu,ni kwa namna gani mkataba uishe mara tu ligi inapokwisha? Na ni nini maana ya matumizi ya TMS kwa timu za VPL na FDL? Na ni kwanini katika utaratibu wa kutumia TMS kuna kipengele cha kuandika muda wa mkataba wa mchezaji na sio fixed time ya mwaka mmoja kama inavyodaiwa kwa timu za daraja la kwanza kama linavyozungumzwa na viongozi wa Yanga? Klabu ya KIMONDO inahoji ni kanuni ipi inayotumika/iliyotumika katika hili?
Kwa suala hili, Timu ya Kimondo isingependa kuona TFF ikipakwa matope kuwa ilishiriki kutoa go-ahead kwa timu ya Yanga kwa kigezo kuwa mchezaji wa ligi daraja la kwanza hawana mikataba, na usajiri wao huishia msimu unapomalizika. Tunaamini kuwa haya ni maelezo yaliyotolewa na uongozi wa Yanga kwa lengo la kutetea maslahi yao.
Kuhusiana na madai yanayotolewa na klabu ya YANGA kuwa klabu ya KIMONDO ilikuwa wapi tangu muda wote huo hadi kuja kuibuka na kudai kuwa mchezaji Geofrey Mwashiuya ni mali mara baada ya kung’ara katika mechi dhidi ya klabu ya Villa ya kutoka Uganda katika uwanja wa Taifa?
Klabu ya KIMONDO inaona hoja iliyotolewa na klabu ya YANGA ni dhaifu na haina mashiko kwakuwa klabu ya KIMONDO isingeweza kukurupuka pasi na ushahidi wowote kuwa klabu ya YANGA imemsajili mchezaji wetu zaidi ya hapo mwanzo kusikia tu kama tetesi katika vyombo vya habari. Kwa kutumia vyombo hivyohivyo vya habari klabu ya KIMONDO ilitoa angalizo dhidi ya timu zote zinazohitaji huduma ya mchezaji huyu zifuate utaratibu unaokubalika ka kuwasiliana na klabu yetu.
Katibu wa Yanga alienda mbali kwa kusema kwamba ,aliandika barua mwezi wanne kutaka kujua status za mchezaji Geofrey Mwashiuya na Mateo Danny Silavwe lakini hadi sasa hakupata majibu. Klabu inahoji kama alijua mchezaji mara ligi iishapo na mkataba unakwisha je alikuwa anaandika barua kutaka kujua endapo Geofrey ana mkataba na KIMONDO katika muktadha upi?na je hiyo barua alimwandikia  nani,na nani alipokea?Katika hili mnaweza kupima maelezo ya klabu ya YANGA dhidi yetu.
Uongozi wa KIMONDO unazidi kusisitiza kuwa mchezaji huyu ana mkataba nasi wa miaka minne na tunawashauri YANGA wafuate utaratibu unaotakiwa katika usajili na si vinginevyo.
Kama ni kweli walimsajili katika dirisha dogo mwezi Oktoba  basi kuna shida kubwa hapa,kwakuwa klabu ya KIMONDO ilimsajili mchezaji huyu mwezi wa nane tarehe 31,2014.Au kama ni kweli walimsajili mwezi wa pili,2015 ilhali KIMONDO ilimsajili mwezi wa nane tarehe 31 basi kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria za FIFA juu ya uhamisho/usajili wa wachezaji.Kwakuwa sheria zinasema mchezaji ataruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu yoyote akiwa amebakiza miezi sita ya kumalizika kwa mkataba wake. Kwa mtizamo wao kuwa mchezaji wa FDL husajiliwa kwa mkataba wa mwaka mmoja mmoja.Izingatiwe kwamba kundi A ambalo klabu ya KIMONDO ilikuwepo mchezo namba moja ulikuwa dhidi ya KIMONDO  na VILLA SQUAD ulichezwa tarehe 11/10/2014 katika uwanja wa CCM –VWAWA MBEYA,mchezaji huyo alicheza akiwa amevalia jezi namba 22. Zaidi alicheza michezo yote mfululizo ya raundi ya kwanza hadi tarehe 20/11/2014.
Swali la kujiuliza,kama kweli mchezaji huyu alikuwa anaishi jangwani kuanzia mwezi Oktoba ,alikuwa anatokea Jangwani kwenda kucheza mechi za KIMONDO au alikuwa anacheza kwa mkopo?Tulitafakari hili kwa pamoja.Juu ya hili kumbukumbu zilizopo katika klabu yetu,Bodi ya Ligi na TFF zinaonyesha mchezaji huyu amecheza mchezo namba 129 wa tarehe 13/02/2015 kati ya KIMONDO dhidi ya MAJIMAJI FC ya Songea akiwa amevalia jezi namba 22.
Pamoja na hilo mchezaji huyu mwezi wa tatu mwaka huu amecheza katika ligi ya MSYETE CUP akichezea timu ya ISANSA BOYS FC  wakicheza na MPITO FC. Mwezi wan ne mwaka huu alikuwa akishiriki katika ligi ya JABU CUP hapo MPEMBA Katika viwanja vya Shule Ya Msingi Katete akiwa na timu ya NANSERE BOYS  FC ya Mpemba dhidi ya CHAPWA FC.
Kama hiyo haitoshi ameshiriki katika ligi ya KIMONDO CUP 13/05/2015 ,Pia tarehe 17/05/2015 amecheza katika ligi ya ZAMBI CUP katika fainali akiwa na ICHENJEZYA FC dhidi ya VWAWA SMALL BOYS. Kama hiyo haitoshi tarehe 24/05/2015 amecheza ligi ya DIWANI CUP  kata ya Halungu katika nusu fainali akichezea timu ya WASA FC  dhidi ya LWATI FC.
Tunajiuliza kwa michezo yote hiyo hiyo katika tarehe mbalimbali za michezo tajwa hapo juu je yote alikuwa anatokea jangwani? Na kama hakuwa anatokea jangwani kipindi chote hicho hawa Yanga wanajua alikuwa anakula,anavaa nini kama walivyodai katika hoja zao.
Katika mkataba wetu na mchezaji kipengele cha nne sehemu c kinachosema;
Katika kipindi chote cha mkataba mchezaji anaweza kufanya majaribio kwa makubaliano ya kimaandishi kutoka kwa klabu ,hivyo basi mchezaji amekiuka kipengele cha nne sehemu c.
Zaidi tunaamini klabu ya YANGA kwa makusudi imevunja kanuni hii ambayo ambayo inasema mchezaji hataruhusiwa kufanya majaribio bila kuwa na kibali au makubaliano ya kimaandishi na klabu yenye mkataba na mchezaji. Kama ambavyo wao YANGA hawakuafikiana na utaratibu uliofanywa na mchezaji wao SIMON MSUVA kwenda kufanya majaribio nchini Afrika ya Kusini ya bila kuwa na kibali kutoka kwao.
Tunapenda kuujulisha umma kuwa KIMONDO ndio klabu ya kwanza kumudu kusajili kwa wakati kwa kutumia mfumo wa TMS. Kwa mujibu wa barua ya pongezi tuliyoandikiwa na TFF ilisema kwamba endapo muda wa tarehe ya mwisho ya ufungaji wa dirisha la usajili usingeongezwa basi ni klabu moja tu ndio ingekuwa imekamilisha usajili kwa wakati nayo ni sisis KIMONDO SUPER SPORTS CLUB. Na pia hili lieleweke wazi kwamba usajili wa 2014/2015 hakukuwa na ujazaji wa fomu ya aina yoyote kwa timu zote za FDL na VPL kama ilivyodaiwa na mchezaji akichagizwa na uongozi alioandamana nao kwenda TFF na katika vyombo vya habari. Kwa nyongeza vitu vilivyotakiwa kuambatanishwa katika usajili ni vivuli vya mkataba,cheti cha kuzaliwa, na cheti cha daktari.Zaidi tumeelekezwa kuwa mfumo huu ndio utatumika tena kwa msimu wa 2015/2016 kuanzia tarehe       15/June hadi August/2015
Tunapenda kuufahamisha umma wa watanzania kuwa usajili wa dirisha dogo ulikuwa November hadi December 2015 na si kama ulivyoelezwa na uongozi wa Yanga kuwa walimsajili katika dirisha dogo la ,mwezi Oktoba.
Zaidi tunaamini Geofrey Bahati Mwashiuya ni mchezaji halali wa KIMONDO na atatumika kwa kipindi cha mkataba kama hakuna klabu itakayokuwa na uhitaji wa huduma yake kwa kufuata taratibu ,kanuni na sheria za usajili. Kama hakutakuwa na sababu nyingine yeyote ya kuvunja mkataba kwa pande zote mbili.
ASANTENI SAANA KWA KUNISIKILIZA

                                                            Imesainiwa na
Elick Ambakisye (0755-708828)
MKURUGENZI
Kimondo Super Sports Club

Dec 29, 2014

LIGI KUU YA VODAOM YAINGIA RAUNDI YA 9




Wakati raundi ya nane ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inakamilika leo (Desemba 29 mwaka huu) kwa mechi tatu, ligi hiyo itaingia raundi ya tisa Januari 3 mwakani kwa mechi tano.

Coastal Union itacheza na JKT Ruvu katika Uwanja wa Mkwakwani, Ruvu Shooting itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mabatini, Azam itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Azam Complex, Stand United itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri wakati Mbeya City na Yanga zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Sokoine.

Ligi hiyo ambayo itachezwa mfululizo (non-stop) hadi itakapomalizika Mei 9 mwakani, itakamilisha raundi ya tisa Januari 4 mwakani kwa mechi kati ya Mgambo Shooting na Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani, na Tanzania Prisons itakayokuwa mwenyeji wa Ndanda kwenye Uwanja wa Sokoine.

Nayo mechi kati ya Mtibwa Sugar na Stand United ambayo jana ilivunjwa na mvua dakika ya 6 imemaliziwa leo ambapo timu hizo zimetoka sare ya bao 1-1.

Wakati huo huo, mechi ya ligi iliyochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex imemalizika kwa wageni Ruvu Shooting kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Ruvu. Bao hilo lilifungwa kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na Hamisi Kasanga.  

MBAO FC YAKAMATA USUKANI SDL
Timu ya Mbao FC ya Mwanza imekamata uongozi wa Kundi B la michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) baada ya jana (Desemba 27 mwaka huu) kuizamisha JKT Rwamkoma ya Mara mabao 2-1.

Kwa matokeo hayo katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mbao FC imeitoa kileleni JKT Rwamkoma baada ya kufikisha pointi tisa kwa kushinda mechi zote tatu dhidi ya Arusha FC, Pamba na JKT Rwamkoma.

Mbao FC inafuatiwa na JKT Rwamkoma yenye pointi sita, Arusha FC pointi sita wakati Bulyanhulu na Pamba zikiwa za mwisho kwa pointi moja kila moja. Kundi hilo litakamilisha mzunguko wa kwanza Januari 3 mwakani kwa mechi kati ya JKT Rwamkoma na Arusha FC, na Bulyanhulu na Mbao FC.

Katika kundi A, Mji Mkuu (CDA) na Singida United ndizo zinazochuana kileleni kwa kufikisha pointi saba kila moja. Timu hizo zinafuatiwa na Milambo yenye pointi nne, Mvuvumwa FC yenye pointi moja wakati Ujenzi Rukwa ni ya mwisho ikiwa haina pointi.

Hata hivyo, Mvuvumwa FC na Milambo ziko nyuma kwa mechi moja. Mechi hiyo ya kukamilisha raundi ya tatu kati ya timu hizo itachezwa kesho (Desemba 29 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Kiluvya United imeendelea kuchachafya kundi C baada ya kushinda mechi zote ne ilizocheza, hivyo kufikisha pointi 12. Inafuatiwa na Mshikamano yenye pointi saba huku Abajalo ikiwa katika nafasi ya tatu kwa pointi 6.

Nafasi ya nne inashikwa na Transit Camp yenye pointi nne, Cosmopolitan yenye pointi mbili ni ya tano wakati Kariakoo ambayo haina pointi ni ya mwisho. Hata hivyo, Cosmopolitan na Kariakoo zina mchezo mmoja mkononi.

Mechi zinazofuata za kundi hilo ni Januari 3 mwakani kati ya Kariakoo na Mshikamano na Mshikamano (Ilulu), Transit Camp na Abajalo (Mabatini), na Cosmopolitan na Kiluvya (Karume).

Kundi D, vinara bado ni Njombe Mji yenye pointi 12 ikifuatiwa na Wenda yenye pointi sita wakati Volcano FC iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi tano. Mkamba Rangers ina pointi nne, Town Small Boys ina pointi moja wakati Magereza FC haina pointi.

Katika kundi hilo leo (Desemba 28 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Town Small Boys na Magereza itakayochezwa Uwanja wa Majimaji mjini Songea.  Januari 3 mwakani kutakuwa na mechi kati ya Town Small Boys na Njombe Mji, Volcano FC na Magereza, na Wenda na Mkamba Rangers.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)