Adverts

Jun 4, 2018

BENKI YA NMB YAJIELEKEZA KUJENGA UWEZO KWA VIKUNDI

Benki ya NMB Tawi la Mbozi na Mlowo kwa pamoja wameelezea nia yao ya kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Mbozi katika kushughulikia changamoto za ukuaji na uaminifu kwa vikundi vya wakulima ili mikopo inayopatikana iwe na tija kiuchumi 
Wakizungumza na menejimenti na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi, Timu ya wataalamu wa benki hiyo wamesema bado jamii ya wananchi wa Mbozi hawajafikiwa vyema na elimu ya Mikopo kiwango ambacho wengi wa wanaojitokeza kukopa  kutokujipanga vyema kulingana na mipango yao.
Wamesema ikiwa halmashauri inaona vyema kutoa huduma zake kupitia vikundi ni vyema wakaishirikisha benki hiyo ili kujenga uwezo na kuandaa wajasiliamali wenye nia ya dhati  ya kujikwamua na umaskini kwanza badala ya kuanzisha programu za hamasa juu ya mikopo mbalimbali bila kuwaandaa kwanza 

VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA VINGI VYAVUKA KIKWAZO KWENYE VIGEZO 2017/2018

Vituo vya kutolea huduma za afya 19 tu kati ya 80 ndivyo vilivyopata nyota sifuri katika tathmini ya mwaka 2017/2018 imefahamishwa.
Wakitoa taarifa ya ukaguzi wa  hali ya vituo hivyo kwa kuzingatia mwongozo wa BRN, Wakaguzi wa wizara ya Afya wamesema kuna ongezeko kubwa la vituo vilivyovuka kutoka nyota sifuri hadi kuingia kwenye nyota moja ikilinganishwa na mwaka 2016.
Kwa mwaka 2016 vituo 45 vilipata nyota 0 kati yake vikiwemo zahanati 45 lakini kwa mwaka huu hali imekuwa tofauti ambapo Zahanati 19 kati yake 16 za serikali zimepata nyota sifuri, zahanati  48 zimepata nyota moja, 8 Nyota Mbili ambapo vimo vituo vya afya na Hospitali ya Misheini ya Mbozi na  Hospitali ya wilaya ya Mbozi imepata Nyota tatu.
Katika mchanganuo huo Zahanati ya Mbaya ambayo ni Binafsi imeshika nafasi ya mwisho kwa kupata wastani wa alama 0.
Katika uchambuzi huo miongoni mwa mapungufu yaliyobainishwa nipamoja na  vituo 63 kati ya 80 kutokuwa na vyoo seti tatu kama mwongozo unavyotaka ambapo inashauriwa kuwa na vyoo vya wanawake, wanaume na watoa huduma (wataalamu) kwenye majengo ya zahanati, aidha kukosekana kwa vyoo rafiki kwaajili ya walemavu na wenye mahitaji maalumu.
Katika ukaguzi huo kulikuwa na jumla ya Maeneo 12 yaliyowekwa kwenye makundi katika ukaguzi yakiangalia uwezo na uendeshaji wa vituo vyenyewe ikiwa ni pamoja na miundombinu yake, utendaji wa wataalamu, Matumizi ya zana, vitendanishi na takwimu za afya zilizopo kituoni katika kupanga mipango ya mbele, ushughulikiaji wa  huduma za dharura, mtazamo wa kumlenga mteja na uwajibikaji.

HALMASHAURI YA WILAYA YA MBOZI YAJIELEKEZA KUFIKIA 100% YA MAKUSANYO

Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi imeagizwa kusimamia ukusanyaji wa mapato yake ya ndani kwa asilimia 100, ili iweze kutekeleza miradi yake iliyopangwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi akiwa na wajumbe wenzake wa kamati ya Fedha ya Halmashauri hiyo ametoa msimamo wa madiwani wakati akizungumza na wananchi kata ya Isansa baada ya kamati hiyo kujiridhisha na ujenzi wa kituo cha afya unaofanywa kwa njia ya Force account.
Amesema wakati zimesalia siku chache kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2017/2018 ni vyema wataalamu wakatambua kuwa Halmashauri ya wilaya haijafanikiwa kutekeleza baadhi ya miradi ya Maendeleo kutokana na mapato kidogo ya ndani ambapo hadi kufikia Juni Mosi Halmashauri imefikia asilimia 78 ya makusanyo yake ya ndani hata hivyo kuna vyanzo vingi zikiwemo leseni za biashara ambazo bado hazijaweza kukusanywa vyema, hivyo mkakati wake kwa sasa ni kujielekeza kukusanya kwenye vyanzo hivyo sambamba na mazao baada ya msimu wa mavuno kuanza.
Kutokana na hatua hizo tayari timu ya mapato ya Halmashauri ya wilaya ya Mbozi imeundwa ikihusisha wataalamu wa idara mbalimbali, huku kamati ya fedha ya Halmashauri hiyo ikikasimiwa majukumu ya kusimamia utendaji wa menejimenti katika kipindi chote ili kuhakikisha kuwa malengo yanafikiwa.
Kwa upande wao wataalamu wameahidi kutekeleza wajibu wao hasa katika suala la makusanyo na kwamba matarajio yao ni kuona kuwa Halmashauri yao inafanya vyema katika utekelezaji wa malengo yake ikiwemo miradi iliyopangwa.