MAREHEMU VITUS THOMAS SWALE
Bwana Vitus Thomas Swale, alizaliwa mwaka 1974 katika kijiji cha Kanikelele huko Lupembe Wilayani Njombe Katika Familia Ya Mzee Thomas Swale.
Marehemu alianza masomo yake ya elimu ya msingi mwaka 1982 na kuhitimu mnamo mwaka 1988 huko huko lupembe.
Baada ya Kuhitimu Elimu ya Msingi alijiunga na elimu ya sekondari katika shule ya Sekondari ya Wavulana ya Malangali kuanzia mwaka 1989 na kuhitimu mwaka 1992. marehemu alijiendeleza na masomo ya kidato cha sita akiwa kama mwanafunzi wa kujitegemea.
Marehemu alisoma kozi mbalimbali na kuhitimu ikiwa ni pamoja na kozi ya Uongozi (Supervisory Management), kisha mwaka 1995 aliajiriwa na kampuni ya Tanganyika Wattle Company Limited akiwa kama Supervisor mpaka mwaka 2006.
Akiwa chini ya kampuni ya Tanganyika Wattle Company Limited pia alifanya kazi na shirika lisilo la kiserikali liitwalo AMREF ambapo alifanya kama PEER HEALTH EDUCATOR katika shirika alilokuwa akifanya kazi.
Mwaka 2007 alijiunga na kituo cha redio cha Uplands Fm Njombe Iringa akiwa mtangazaji wa Kawaida, na kutokana na utendaji wake mzuri wa kazi alipandishwa ngazi na kushika nafasi ya Umeneja wa redio mpaka kifo kinamkuta tarehe 09 January 2011 majira ya saa kumi na mbili za jioni katika hospitali ya Kibena alikopelekwa baada ya kuanguka ghafla akiwa ofisini kwake.
Kifo chake kimeacha pengo kubwa sio tu katika kituo cha redio bali kwa jamii nzima ambayo ilikuwa inahusiana naye katika shughuli za kila siku.
Marehemu atakumbukwa sana kwa uhodari wake katika kazi mbalimbali akiwa kama meneja na pia katika uendeshaji wa vipindi mbali mbali vya redio ikiwa ni pamoja na kipindi cha SAYARI YA UPAKO na WAZO TETE
Marehemu ameacha mjane na watoto wanne kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa msemaji wa familia yake.
Kama familia na kituo cha redio uplands fm iliyopo wilayani Njombe mkoani Iringa tunapenda kutoa shukrani za dhati kwa wananchi wote, uongozi wa kitongoji cha kihesa, wasikilizaji wa Uplands fm, wadau, wafanyakazi wa redio na watu wote walioshiriki nasi kwa namna moja ama nyingine katika kumsindikiza marehemu kwenye nyumba ya milele.
Uongozi wa Uplands fm pamoja na wafanyakazi umetoa rambi rambi ya kiasi cha sh. Milioni moja na laki mbili ili kusaidia shughuli mbalimbali za mazishi ya marehemu.
Hii ndio Historia fupi ya marehemu Vitus Thomas Swale.kama ilivyosomwa nami Hamphrey Milinga Mkurugenzi Mtendaji wa Uplands fm. Bwana Alitoa, Na Bwana Ametwaa.....Jina La Bwana Libarikiwe.
Mungu Ailaze Roho Ya Marehemu Mahali Pema Peponi....Amina
Neno La Mungu Kwa Familia ya Marehemu.
Wafilipi 4:12:13.
“Najua kudhiliwa tena najua kufanikiwa katika hali yoyote katika mambo yoyote. Nimejifunza kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza haya yote katika yeye anitiaye nguvu”.
"
indaba2010