Adverts

Feb 27, 2011

BOSS WA MOHAMED ENTERPRISES IRINGA MATATANI KWA UCHAFU

kaimu OCD Iringa akiwa na viongozi wa Manispaa baada ya kumtia hatiani meneja wa METL,Iringa
HALMASHAURI ya manispaa ya Iringa imezindua siku ya usafi kwa kila jumamosi ya kwanza ya mwanzo wa mwezi ikiwa ni pamoja na kuweka sheria kali kwa wanaotupa taka ovyo na kujisaidia maeneo yasiyo rasmi kuwa adhabu ya papo kwa papo itakuwa ni shilingi 50,000. Huku kaimu meneja wa kampuni ya Mohamed Enterprises Tanzania Ltd (METL) mkoani Iringa Ivani Ole Mganga akifikishwa polisi kwa kuwashambulia kwa lugha chafu viongozi wa Halmashauri hiyo wakiongozwa na Mstahiki meya, kaimu mkurugenzi na mkuu wa polisi wilaya ambao walikuwa katika kampeni za usafi jirani na ofisi za kampuni hiyo eneo la Mlandege. Kaimu meneja huyo wa kampuni hiyo METL ,Mganga alikamatwa na polisi majira ya saa 4.02 asubuhi akiwa nje ya ofisi yake baada ya uongozi huo wa Manispaa ya Iringa kumhoji sababu ya kuacha mazingira ya ofisi yake katika hali ya uchafu na badala ya kuwajibu vizuri alianza kuwatolea lugha za matusi kabla ya kaimu mkuu wa polisi wilaya kuagiza askari waliokuwepo eneo hilo kumkamata na kumfikisha kituoni. Akizungumza katika uzinduzi siku ya usafi katika manispaa ya Iringa katika maadhimisho yaliyofanyika kwenye kata ya Kwakilosa mstahiki meya wa Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi alisema kuwa idadi kubwa ya wakazi wa Manispaa hiyo wamekuwa na jeuri kubwa pindi wanapoelezwa juu ya utunzaji wa mazingira . Hata hivyo alisema kukamatwa kwa meneja huyo wa kampuni ya METL ni fundisho kwa wamiliki wengine wa kampuni mjini Iringa na wananchi wa mji huo ambao wamekuwa wakishindwa kuheshimu sheria ya usafi na kuchafua ovyo mazingira yao. Mwamwindi alisema kuwa kuanzia sasa uongozi wa manispaa ya Iringa utaendelea kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kuchafua mazingira kusudi ama kushindwa kuweka mazingira katika hali ya usafi . 'Ujue huyo meneja wa METL kutokana na kufanya kazi katika kampuni ya mwarabu na yeye amejiona ni Mwarabu na kuanza kuleta lugha chafu mbele ya wananchi na viongozi kwa kujiona yupo juu ya sheria....sasa tumeamua sheria hii kuanza kwake kama fundisho kwa wengine' Alisema kuwa lengo la kuweka sheria kali za uchafu ni kutaka manispaa ya Iringa kuja kushika nafasi ya kwanza kiusafi katika Tanzania pia kuepusha magonja ya milipuko kama kipindu pindu na magonjwa mengine ya milipuko . Alisema Meya Mwamwindi kuwa wapo baadhi ya watu wanaoendelea kuchafua mazingira ovyo katika maeneo yao kinyume na sheria ndogo za mji ambazo zinapiga marufuku uchafuzi wa Mazingira na kuwa kutokana na sheria ya sasa adhabu kali imewekwa kwa kundi ,ama mtu yeyote atakayebainika akichafua mazingira kusudi. Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa Mashaka Luhamba alisema kuwa tayari elimu kwa wananchi wa Manispaa hiyo imeanza kutolewa kupitia vyombo vya habari ili kila mkazi wa mji wa Iringa kuitambua vizuri sheria hiyo na pale atakapokwenda kinyume asilalamike kuadhibiwa . Pia alisema kuanzia sasa ni marufuku mifugo kuchungiwa katikati ya mji pia marufuku mtu kutupa taka ovyo kama vocha za simu na kuwa sheria hiyo pia itawabana wamiliki wa nyumba za kuishi na zile za wageni watakaokutwa wanatiririsha maji machafu ovyo. Nao wakazi wa kata ya Kwakilosa ambao walishiriki katika uzinduzi huo wamepongeza jitihada hizo za manispaa ya Iringa katika kumwajibisha meneja huyo wa METL Iringa kwa kuonyesha jeuri wakati wa utekelezaji wa sheria hiyo na kuwa kutokana na mkakati huo upo uwezekano wa mazingira ya mji wa Iringa kuboreshwa zaidi japo waliomba kwa upande wa Manispaa kuhakikisha gari ya taka taka inafika mapema kusomba taka zinazohifadhiwa katika vituo.
"