Feb 2, 2011
Wakamatwa kwa kumdhalilisha rais
Wakamatwa kwa kumdhalilisha rais: "JESHI la Polisi jijini Dar es Salaam wanawashikilia watu kadhaa wakiwamo maafisa waandamizi wa serikali wakiwahusisha na kusambaa kwa picha za kupika zinazomdhalilisha Rais Jakaya Kikwete.
Habari za uhakika ambazo Mwananchi imezipata zinaeleleza kuwa kwa takribani wiki moja sasa, polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama wamekuwa wakiendesha operesheni ya kuwakamata watu wanaoaminika kusambaza kwa kutumia mtandao wa intaneti picha ambazo kwa kiasi kikubwa zinamdhalilisha rais.
Siku ya Jumatatu, watu waliovalia nguo za kiraia na kujutambulisha kama maofisa usalama kutoka makao makuu ya polisi walivamia ofisi za Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) na kuwachukua wafanyakazi watatu kutoka taasisi hiyo ya uhifadhi mazingira kwa mahojiano.
Mwananchi lilifanikiwa kupata majina ya watu watatu (majina yao tunayahifadhi kwa sasa) ambao wote wanafanya kazi katika ofisi hizo wakichukuliwa na polisi siku ya Jumatatu. Hadi tunakwenda mitamboni jana wafanyakazi hao walikuwa bado mikononi mwa polisi kwa mahojiano.
Ndugu wa mmoja wa waliokamatwa alidai kustushwa na kukamatwa kwa dada yake huku akisisitiza kuwa anaamini ndugu yake hahusiki kwa namna yoyote kusambaza picha hizo. “Dada yangu hana hatia kwenye hili…nakuhakikishia hana hatia. Polisi wasilazimishe kuwa wao ni wakosaji wakati inawezekana wametumiwa tu picha hizo. Nadhani in vema polisi wakawatafuta wanaopika picha hizo,” alisema ndugu huyo aliyeomba asitajwe jina.
Mtumishi mwingine wa NEMC amelieleza Mwananchi wakati likifuatilia taarifa hizo kuwa wafanyakazi wengi wanestushwa na kusikitishwa na kukumatwa kwa wenzao waliowaelezea kuwa ni waaadilifu waliotukuka.
Taarifa zinaeleza pia kuwa polisi jana mchana walimwita makao makuu mmoja wa maofisa waandamizi wa baraza hilo, kwa mahojiano. Mpaka jana jioni kigogo huyo alikuwa bado akihojiwa na polisi.
Mtazamo wa kisheria kuhusu kukamatwa huko haujawa wazi sana ingawa baadhi ya waliohojiwa wanasema sheria za Tanzania kuhusiana na mawasiliano ya intaneti ama hazipo kabisa au hazieleweki kwa wananchi wa kawaida ambao wengi wao hutumiwa tu picha hizo.
Vyanzo vyetu pia vimethibitisha kuwa watu wengi zaidi tayari wamekwishakamatwa na polisi juu ya suala hilo wakati polisi wakijaribu kujua chanzo halisi cha picha hizo zinazoshambulia utu wa Rais.
Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Peter Kivuyo amethibitisha kuwa jeshi la polisi linawashikilia baadhi ya watu kuhusiana na suala hilo.
“Ni kweli lakini nadhani nahitaji muda zaidi kufanya mazungumzo na wewe juu ya suala hili. Ni jambo sensitive (nyeti) sana. Nakushauri nipigie kesho asubuhi. Kwa sasa siko katika nafasi nzuri kulizungumzia hili,” alisema Kivuyo.
Mkurugenzi wa makosa ya jinai (DCI) Manumba alisema hakuwa na taarifa juu ya suala hilo kwani yuko likizo.
Kukamatwa kwa watu hao kunaonekana kuwa ni moja ya hatua za wazi kuchukuliwa na jeshi la polisi kumaliza kusambazwa kwa picha hizo zinazoaminika kuandaliwa na baadhi ya watanzania waishio nje ya nchi.
Watu waliozungumza na Mwananchi kuhusiana na suala hilo wamekiri kuogezeka kwa usambazaji wa picha zinazomdhalilisha, si Rais peke yake, bali hata watanzania wa kawaida huku wakitahadharisha kuwa uchunguzi wa polisi lazima ulenge katika kuwakamata wapikaji wa picha hizo na sio watu wanaotumiwa bila ridhaa yao.
“Hizi email zimekuwa zikisambwazwa kwa zaidi ya miaka mitatu sasa na watu wengi wanazipokea kutoka vyanzo mbalimbali.
Nadhani ni vizuri kwa polisi kuwatafuta watengenezaji wa picha hizo kuliko kuwasaka watu wanaozipokea,” alisema mkazi wa jiji aliyeomba kutotajwa jina gazetini.
Hii si mara ya kwanza kwa polisi kutangaza kufanya operesheni kama hii. Mwezi Juni 2009, polisi walitangaza kuwa wameomba msaada kutoka polisi wa kimataifa Interpol wakijaribu kuwasaka wamiliki wa blog maarufu ya Ze utamu ambayo pia ilisambaza picha kama hizo.
Mtandao ambao kwa sasa umefungwa baada ya kupigiwa kelele za kuwadhalilisha watu wengi ulipata umaarufu kwa kuchapisha picha za Watanzania maarufu waishio ndani na nje ya nchi wakiwa uchi na maelezo yaliyolenga kuwadhalilisha.
Licha ya kuvuta watazamaji wengi, blog hiyo ambayo pia ilitoa maoni juu ya maisha binafsi ya watu, ilipingwa vikali na watanzania wengi kwa kutofanana na mila, desturi and utamaduni wa watanzania."