Askofu Ruwai`chi (pichani) alisema Kanisa Katoliki halikiteulii chama chochote cha siasa mgombea na akakipa angalizo CCM akitaka kijidodose juu ya sababu zilizomfanya Dk Willbrod Slaa kukihama na sasa kuonekana kama ni mtu anayekichanganya akili na kutaka iache alichokiita propaganda zenye malengo ya kuwagawa watu katika misingi ya dini.
“Kama Slaa (Dk Willbroad Slaa) alikuwa mwanaCCM akaikimbia. Sasa jifunzeni na kukumbuka historia, CCM wana mchango gani katika hilo la Dk Slaa kuikimbia, wakijibu swali hilo itakuwa vizuri sana,” alisema akisisitiza.Askofu Ruwai’chi alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Parokia ya Kibaigwa, Dodoma muda mfupi baada ya kumpokea Askofu mteule wa Jimbo Katoliki la Dodoma, Mhashamu Gervas Nyaisonga ambaye atasimikwa rasmi leo mjini Dodoma.
Kuhusu Kanisa Katoliki kudaiwa kuwa limekuwa likikiunga mkono Chadema, Askofu Ruwai’chi alisema kuwa hakuna ukweli wowote kuhusu uvumi huo na kwamba kauli hizo zimekuzwa na baadhi ya wanaCCM ambao wamekosa sera na kukurupuka kutoa kauli zisizo za msingi.
“Hizo ni kauli danganya toto, Kanisa halina chama, ila likibidi kuzungumza litazungumza kama lilivyokuwa likifanya kwa maslahi ya watu wote. Viongozi wa dini wasipozungumza watakuwa hawalitendei haki taifa, wanapaswa kusimamia haki pale inapoonekana kupotoshwa, kanisa halina chama,” alisema Askofu huyo.Alisema Chadema ni chama chenye mkusanyiko wa watu wa dini na madhehebu yote, hivyo watu watumie akili zao kutafuta ukweli wa uvumi huo aliosema ni wa kupotosha.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki nchini alisema kila mtu ana wajibu wa kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa njema. Akaeleza kushangazwa kwake na wachache wanaotaka kupandikiza mbegu ya udini ambayo alisema kimsingi haipo nchini.
Alisema kauli kama hizo alizoziita za kichochezi pia zinajenga swali kuwa, huenda CCM ni chama cha watu fulani, lakini akasema kuwa wao viongozi wa dini na kanisa kwa ujumla kazi yao ni kuhakikisha maslahi ya taifa hayachezewi wala hayaendi kiholela, akisisitiza kuwa ni haki ya kila mtu kuwa na mtazamo tofauti wa kisiasa muhimu asivunje sheria.
Huku akisisitiza kuwa Tanzania haiendeshwi katika misingi ya falsafa za kidini wala madhehebu, Askofu Ruwai’chi alisema kuwa viongozi wa dini zote nchini wanapaswa kuzungumza na kukemea dosari za kiutendaji na kiuwajibikaji zinazofanywa na baadhi ya viongozi na watumishi wa umma na kwamba bila hivyo itakuwa ni kutowatendea haki Watanzania.
Alisema viongozi wa dini wanapaswa kuzungumzia matatizo yaliopo nchini, kuhamasisha haki, ukweli, amani na kushughulikia maendeleo ya watu wote bila kuogopa wanaowabeza na kutaka kuwaziba midomo kwa kisingizio kuwa wanaingilia Serikali.
“Kuzungumza siyo kuingilia, viongozi wa dini wana wajibu wa kutoa kauli na kuwashuhudia watu mambo mbalimbali yanayotokea katika nchi, wasipoongea watakuwa hawalitendei haki Taifa,” alisema Askofu Mkuu Ruwai’chi.
Askofu Ruwaichi alisema kuwa viongozi wa dini mbali na kutunza dini, lakini wana wajibu mkubwa wa kusimamia mustakabali wa taifa kwa kuhakikisha wanakemea na kusemea mienendo ya kiovu ambayo kwa namna moja au nyingine, inaweza kuvuruga amani na umoja wa kitaifa.
Askofu mteule Nyaisonga atasimikwa leo katika Kanisa Kuu la Paulo wa Msalaba Mjini Dodoma na Rais Jakaya Kikwete pamoja na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na viongozi wengine wa dini na madhehebu mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria.
Juzi, mamia waumini wa Kanisa katoliki walijitokeza na kuandamana kwa ajili ya mapokezi ya askofu huyo mteule aliyewasili majira ya saa 7:00 mchana Kibaigwa, Dodoma akitokea Mbeya ambako alikuwa akitumika katika shughuli za kitume akiwa Padri Daraja la Pili.
"