Adverts

Aug 21, 2011

UCHUNGUZI WA MOTO ULIOUNGUZA NYUMBA YA KAPT JOHN KOMBA WAENDELEA.

Kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda.
Na Stephano Mango ,Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma tayari limeshaanza kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio la ajari ya moto ulioteketeza nyumba ya Mbunge wa jimbo la Mbinga Magharibi Kapteni John Komba iliyokuwa na thamani ya sh. Milioni 150.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alisema kuwa nyumba ya Kapteni Komba iliyoteketea kwa moto Agosti 15 mwaka huu majira ya saa 11 arfajiri ilikuwa na mali ambayo thamani yake bado haijafahamika licha ya kuwa mmiliki wa nyumba hiyo ameshatoa taarifa kuwa ilikuwa na thamani ya sh. Milioni 150.
Mbali na thamani ya vitu vilivyokuwemo kwenye nyumba hiyo pia afisa masoko wa benki ya wananchi Mbinga (MCB) Emanuel Kumburu (38) aliyekuwa ni mmoja wa wapangaji inadaiwa amepoteza sh. Milioni 4030,000 pamoja na nyaraka mbalimbali za benki hiyo ambazo zilikuwa zimehifadhiwa kwenye chumba alichopanga.
Kamanda huyo alisema kutokana na hali hiyo tayarri polisi imeshaanza kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli halisi wa tukio hilo kwani upo uvumi kwamba inasadikiwa kuwa kuna watu wasiofahamika walichoma nyumba hiyo kwa kutumia mafuta ya petroli na licha ya kuwa awali ilibainika kuwa chanzo kilikuwa ni itilafu ya betri za umeme juwa (Solar )ambazo zilisababisha kuwaka moto na kuteketeza nyumba hiyo.
Kwa upande wake Mbunge huyo Kapteni Kaomba alieleza kuwa thamani ya mali zilizokuwepo kwenye nyumba hiyo ni vigumu kuijuwa haraka hivyo alisema kuwa anahitaji apatiwe muda mzuri ndipo ataweza kujuwa idadi ya mali zilizotekete kwa moto ambazo zilikuwa kwenye nyumba hiyo.
Capt Komba alisema kuwa anaamini kuwa jeshi la polisi ni chombo cha dola ambacho kinauwezo wa kufanya uchunguzi zaidi na kubaini chanzo cha tukio hilo hivyo shughuli hiyo anaiachia jeshi la polisi liendelee kufanyia uchunguzi zaidi.