TANGAZO LA UGAWAJI WILAYA, LATOLEWA UFAFANUZI NA PINDA
- Asaini tangazo la serikali lililochakachuliwa
RAIS Jakaya Kikwete amedanganywa tena na baadhi ya watendaji wake,
akasaini tangazo lililochakachuliwa. Septemba 5 mwaka huu, Kikwete
alisaini tangazo la kusudio la uanzishaji wa wilaya mpya ya Butiama,
lakini katika namna ya kushangaza, sasa inaonekana eneo la wilaya mpya
ni Nyamisisi.
Hali hiyo inayotia fedheha kwa Rais wa nchi, imebainika juzi wakati
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipofika Butiama kuzuru kaburi la Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Pinda alilazimika kuwatuliza wakazi wa eneo hili waliotaka kujua sababu
za msingi za Rais kubadili msimamo wake na kuhamishia makao mapya
yaliyotakiwa kuwa Butiama na kuyapeleka Nyamisisi.
Pinda alikiri bayana kuwa Rais alisaini tangazo hilo akijua kuwa
kilichoandikwa ni makao makuu kuwa Butiama bila kujua eneo lililoandikwa
ni Nyamisisi.
“Hata kama kuna mtu alitaka makao makuu yawe Nyamisisi, kwa kweli
haikupaswa hiyo Nyamisisi kuchomekwa hivyo. Hata mngeniuliza mimi makao
makuu yawe wapi, ningesema lazima yawe Butiama tu,” alisema Pinda na
kushangiliwa.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema tangazo hilo lilikuwa na makosa
kutokana na kutaja eneo la makao makuu tofauti na lile lililopendekezwa.
Pinda alisema mpango wa serikali ulikuwa ni makao makuu ya wilaya hiyo
yawe katika kijiji cha Butiama ili kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati
Mwalimu Julius Nyerere.
Akijibu malalamiko ya wakazi wa Butiama, walioingia katika eneo la
nyumba hiyo, wakimtaka atamke kuwa makao makuu yatakuwa Butiama, Pinda
alisema:
“Hili la Butiama kwa kweli linaleta manenomaneno. Sisi serikalini
tulidhani ukiwa na wilaya ya Butiama na makao makuu ni lazima yawe
Butiama, ili tumuenzi Baba wa Taifa.
Hata hivyo, alisema pamoja na tangazo hilo kuchomekwa neno Nyamisisi,
bado mtu aliyefanya hivyo hajafanikiwa, kwani tangazo hilo sio uamuzi wa
mwisho wa kuhusu suala hilo.
Aliwataka wananchi wa Butiama kulichukulia tangazo hilo kuwa ni
pendekezo tu ambalo wanapaswa kulitolea maoni yao kuhusu kulikubali au
kulikataa na kwamba maamuzi ya mwisho kuhusu wapi yawe makao makuu ya
wilaya hiyo yatatokana na maoni ya wananchi wenyewe.
Alisisitiza kuwa Butiama ikiwa wilaya sio tu huduma za msingi
zitaboreshwa na kuwapa watu sababu ya kwenda wilayani hapo, bali pia
itawapa sababu ya kwenda kuzuru nyumbani kwa Hayati Baba wa Taifa.
Pinda pia alimpa fursa mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere,
kutoa kauli yake kuhusu suala hilo, ambaye alisema yeye asingependa
kuliingilia suala hilo.
“Hili suala halina tatizo, ninyi na wananchi wote mtakavyoamua ndivyo iwe hivyohivyo,” alisema Mama Maria. KUTOKA JAMII FORUMS