Wakati raundi ya nane ya
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inakamilika leo (Desemba 29 mwaka huu) kwa mechi
tatu, ligi hiyo itaingia raundi ya tisa Januari 3 mwakani kwa mechi tano.
Coastal Union itacheza
na JKT Ruvu katika Uwanja wa Mkwakwani, Ruvu Shooting itaikaribisha Kagera
Sugar kwenye Uwanja wa Mabatini, Azam itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar katika
Uwanja wa Azam Complex, Stand United itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja
wa Jamhuri wakati Mbeya City na Yanga zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa
Sokoine.
Ligi hiyo ambayo
itachezwa mfululizo (non-stop) hadi itakapomalizika Mei 9 mwakani, itakamilisha
raundi ya tisa Januari 4 mwakani kwa mechi kati ya Mgambo Shooting na Simba
kwenye Uwanja wa Mkwakwani, na Tanzania Prisons itakayokuwa mwenyeji wa Ndanda
kwenye Uwanja wa Sokoine.
Nayo mechi kati ya
Mtibwa Sugar na Stand United ambayo jana ilivunjwa na mvua dakika ya 6
imemaliziwa leo ambapo timu hizo zimetoka sare ya bao 1-1.
Wakati huo huo, mechi ya
ligi iliyochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex imemalizika kwa
wageni Ruvu Shooting kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Ruvu. Bao hilo
lilifungwa kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na Hamisi
Kasanga.
MBAO FC YAKAMATA USUKANI
SDL
Timu ya Mbao FC ya
Mwanza imekamata uongozi wa Kundi B la michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL)
baada ya jana (Desemba 27 mwaka huu) kuizamisha JKT Rwamkoma ya Mara mabao 2-1.
Kwa matokeo hayo katika
mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mbao FC imeitoa kileleni JKT
Rwamkoma baada ya kufikisha pointi tisa kwa kushinda mechi zote tatu dhidi ya
Arusha FC, Pamba na JKT Rwamkoma.
Mbao FC inafuatiwa na
JKT Rwamkoma yenye pointi sita, Arusha FC pointi sita wakati Bulyanhulu na
Pamba zikiwa za mwisho kwa pointi moja kila moja. Kundi hilo litakamilisha
mzunguko wa kwanza Januari 3 mwakani kwa mechi kati ya JKT Rwamkoma na Arusha
FC, na Bulyanhulu na Mbao FC.
Katika kundi A, Mji Mkuu
(CDA) na Singida United ndizo zinazochuana kileleni kwa kufikisha pointi saba
kila moja. Timu hizo zinafuatiwa na Milambo yenye pointi nne, Mvuvumwa FC yenye
pointi moja wakati Ujenzi Rukwa ni ya mwisho ikiwa haina pointi.
Hata hivyo, Mvuvumwa FC
na Milambo ziko nyuma kwa mechi moja. Mechi hiyo ya kukamilisha raundi ya tatu
kati ya timu hizo itachezwa kesho (Desemba 29 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Lake
Tanganyika mjini Kigoma.
Kiluvya United
imeendelea kuchachafya kundi C baada ya kushinda mechi zote ne ilizocheza,
hivyo kufikisha pointi 12. Inafuatiwa na Mshikamano yenye pointi saba huku
Abajalo ikiwa katika nafasi ya tatu kwa pointi 6.
Nafasi ya nne inashikwa
na Transit Camp yenye pointi nne, Cosmopolitan yenye pointi mbili ni ya tano
wakati Kariakoo ambayo haina pointi ni ya mwisho. Hata hivyo, Cosmopolitan na
Kariakoo zina mchezo mmoja mkononi.
Mechi zinazofuata za
kundi hilo ni Januari 3 mwakani kati ya Kariakoo na Mshikamano na Mshikamano
(Ilulu), Transit Camp na Abajalo (Mabatini), na Cosmopolitan na Kiluvya
(Karume).
Kundi D, vinara bado ni
Njombe Mji yenye pointi 12 ikifuatiwa na Wenda yenye pointi sita wakati Volcano
FC iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi tano. Mkamba Rangers ina pointi nne, Town
Small Boys ina pointi moja wakati Magereza FC haina pointi.
Katika kundi hilo leo
(Desemba 28 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Town Small Boys na Magereza
itakayochezwa Uwanja wa Majimaji mjini Songea. Januari 3 mwakani kutakuwa
na mechi kati ya Town Small Boys na Njombe Mji, Volcano FC na Magereza, na Wenda
na Mkamba Rangers.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO
LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)