Adverts

Nov 4, 2010

WALIOTEMBEZA JENEZA TUNDUMA WATINGA MAHAKAMANI

Vijana wawili wamepandishwa jana kwenye Mahakama ya mwanzo ya Vwawa wilayani Mbozi kwa kosa la kutembeza jeneza lililofunikwa bendera ya chama cha mapinduzi pamoja na msalaba katika mji mdogo wa Tunduma baada ya kutangazwa ushindi wa kiti cha ubunge kupitia chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA jimbo la Mbozi Magharibi.


Waliopandishwa kizimbani ni Selemani Ibrahimu maarufu kama mwarabu na Maneno Halongo wote wakazi wa mji wa Tunduma.


Wakisomewa shitaka lao mbele ya Mh hakimu wa mahakama ya mwanzo Vwawa Ismail Karuta, mwendesha mashitaka wa polisi koplo Pascal Mkondya aliieleza mahakama kuwa mnamo Novemba 2 mwaka huu saa 7 mchana katika mji wa Tunduma watuhumiwa walibeba sanduku mfano wa jeneza na bendera ya CCM wakiimba nyimbo za mazishi kitendo ambacho kilikuwa cha uvunjifu wa amani.

Alisema chini ya sheria ya maadili ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani namba 124 ya 1985 sura ya 342 kifungu kidogo cha 2 d pamoja na tangazo la serikali namba 273 la agosti 2010 ambalo linakataza vitendo vyenye lengo la kudhalilisha ama kukikashifu chama kingine.



Pamoja na kukana shitaka hilo, washitakiwa hao walishindwa kutimiza masharti ya dhamana baada ya hakimu Ismail Karuta kuwataka kudhaminiwa na watu watatu ambao ni watumishi wa serikali pamoja fedha kwa maneno kiasi cha shilingi 500,000/=. Watuhumiwa walipelekwa mahabusu hadi novemba 17 kesi yao itakapoanza kusilikilizwa.



Danny tweve Mbozi

indaba2010